PROFESA LIPUMBA AMTAKA WARIOBA ASIHARAKISHE MCHAKATO WA KATIBA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/06/profesa-lipumba-amtaka-warioba.html
![]() |
| Profesa Ibrahim Lipumba. |
Mwenyekiti wa Chama Cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, amemtaka Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba kutoharakisha mchakato huo hadi pale itakapopatikana rasimu ya Katiba ya Tanzania Bara.
Pamoja na kutoa kauli hiyo katika mkutano wake na waandishi wa habari jana, Mwenyekiti huyo pia alielezea kasoro 17 zilizopo katika Rasimu mpya.
Alionesha wasiwasi kuhusu namna Katiba ya Serikali ya Muungano, itakavyokuwa kutokana na Rasimu ya Katiba ya sasa kutobainisha ipasavyo masuala ya uratibu wa Sera za uchumi.
Kutokana na hayo, Mwenyekiti huyo, ambaye pia ni mchumi alisema kuna hatari ya Watanzania kupata Katiba ya nchi isiyotokana na maoni yao kwa mujibu wa sheria na kumtaka Jaji Warioba kwenda taratibu na kuangalia kila kitu kwa kina na kuona athari zake.
“Pendekezo langu la msingi ni kwamba, kura ya maoni isubiri kukamilishwa kwa Rasimu ya Katiba ya Tanzania Bara na zote zikajadiliwa na wananchi kwa pamoja,” alisema Lipumba na kuongeza kuwa hana pingamizi kwa Wajumbe wa Tume wa Tanzania Bara kuandaa Rasimu ya Katiba ya Tanzania Bara, na wajumbe wa Zanzibar waandae mapendekezo ya marekebisho ya Katiba ya Zanzibari ili isikinzane na Katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Aidha alisema muda wa kuyatekeleza maamuzi na kubadilisha sheria ili ifuate matakwa ya Katiba mpya kabla ya uchaguzi mkuu wa 2015 haupo hivyo ni vyema kukawa na utaratibu.
‘’ Serikali imeeleza kuwa haina nia na Rais Kikwete hataki kabisa kujiongezea muda kwa kisingizio cha kukamilisha utaratibu wa Katiba mpya. Wananchi pia wamechoka wanataka mabadiliko,’’ alisema Profesa Lipumba na kupongeza pamoja na hayo kuharakisha bila kuangalia uhalisia itakuwa kuwanyima watu haki yao.
Akichambua zaidi alisema chama chake kimebaini maeneo 17 ndani ya rasimu hiyo iliyoweka Serikali tatu ambayo haijabainisha utekelezaji sahihi wa Serikali ya Muungano kutokana na ukweli kuwa haijapewa nyenzo za kusimamia, hasa masuala ya uchumi.
Alisema kasoro kubwa ya Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano ni kwamba haina nyenzo za kutimiza malengo muhimu ya Katiba yenyewe.
“Ibara ya 6(b) imeeleza kuwa “lengo kuu la Serikali litakuwa ni maendeleo na ustawi wa wananchi.” Mambo ya uchumi yote isipokuwa Benki Kuu na sarafu hayamo katika orodha ya mambo ya Muungano. Hata suala la uratibu wa sera za uchumi halimo,” alisisitiza.
Alisema katika Ibara ya 7(2) inaeleza kuwa mamlaka ya nchi na vyombo vyake vinawajibika kuelekeza sera na shughuli zake zote kwa lengo la kuhakikisha kwamba shughuli zinazofanywa zinatekelezwa kwa njia ambazo zitahakikisha utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla.
“Pia mamlaka hizo zinawajibika kuhakikisha ardhi inalindwa, kutunzwa na kutumiwa na wananchi wa Tanzania kwa manufaa, maslahi na ustawi wa kizazi cha sasa na vizazi vijavyo, maendeleo ya uchumi wa Taifa yanapangwa na kukuzwa kwa ulinganifu na kwa namna itakayonufaisha wananchi wote…Serikali ya Muungano haina nyenzo ya kusimamia mambo hayo yote,” alisisitiza Lipumba.
Alisema katika eneo la utekelezaji wa malengo ya taifa, rasimu hiyo inaelezwa kuwa Serikali itatoa taarifa bungeni si chini ya mara moja katika kila mwaka, kuhusu hatua zilizochukuliwa na mamlaka ya nchi ili kuhakikisha utekelezaji wa malengo ya Taifa yaliyoainishwa katika Katiba hiyo.
Pia katika eneo la uchumi imeandikwa Serikali itachukua hatua zinazofaa ili kuwaletea wananchi maisha bora kwa kuondoa umasikini, kuhakikisha kwamba shughuli za Serikali zinatekelezwa kwa njia zitakazohakikisha kuwa utajiri wa Taifa unaendelezwa, unahifadhiwa na unatumiwa kwa manufaa ya wananchi wote kwa jumla.
Alisema kihalisia Katiba haizungumzii taasisi yoyote ya kukusanya kodi. Jambo la saba la Muungano ni Ushuru wa bidhaa na mapato yasiyo ya kodi yatokanayo na mambo ya Muungano. Mambo sita ya Muungano hayalipi ushuru wa bidhaa.
“ Biashara siyo jambo la Muungano kwa hiyo ushuru wa forodha, kodi za ongezeko la thamani (VAT), excise duty, kodi ya mauzo haziwezi kuwa suala la Muungano,” alisema Lipumba na kuongeza kuwa katika mazingira hayo Serikali imenyimwa uwezo wa kiuchumi.
Mambo mengine aliyozungumza ni Katiba kutamka wazi maslahi ya kiafya ya mama wajawazito na watoto.
Pia alizungumzia masuala ya kuzuia mtu kumnyonya mtu mwingine, kuweka mazingira bora kwa ajili ya kuanzisha na kuendeleza vyombo vya uwakilishi wa wakulima, wafugaji na wavuvi, kuweka mazingira bora ya kufanya biashara na kukuza fursa za uwekezaji.
“Yote haya na mengine yakiwemo kuweka mazingira bora kwa ajili ya kukuza kilimo, ufugaji na uvuvi kwa kuhakikisha kuwa wakulima, wafugaji na wavuvi wanakuwa na ardhi na nyenzo kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao… siyo ya Muungano, Serikali ya Muungano itawezaje kutoa taarifa bungeni kwa mambo ambayo haiyasimamii,” alisema.
Katika eneo la Bunge, Lipumba, alisema rasimu hiyo imeshindwa kufafanua namna ya upatikaji wa majimbo zaidi ya kutoa tafsiri ya jumla kuwa kila mkoa utakuwa na jimbo la uchaguzi na wilaya kwa upande wa Zanzibar ambapo kila mkoa utakuwa na wawakilishi wawili.
Eneo la Urais, mwenyekiti huyo, alipinga sifa ya kuwa na mgombea urais mwenye shahada ya kwanza huku akionya kuwa kuna hatari ya nchi kuingia katika uchakachuaji wa vyeti hasa kwa wagombea wengi wa nafasi hiyo.
“Hatari ya jambo hili kubwa sana kwani linaweza kutotoa fursa kwa watu ambao wana sifa za uongozi lakini hawana shahada ya kwanza,” alisema Lipumba.
Profesa Lipumba katika taarifa yake ya uchambuzi alisema pia Katiba haina muongozo wowote wa michango toka washirika wa Muungano na kuongeza kuwa kama ikipitishwa italeta mgogoro mkubwa wa fedha za kuendeshea Serikali ya Muungano na hatma yake itakuwa Muungano kuvunjika.
Alisema katika mambo ya uchumi Tume haikufanya uchambuzi wa kina wa kuwa na Katiba inayojenga mazingira mazuri ya kukuza uchumi unaoleta maendeleo kwa wote.
“Katiba haiibani Serikali iwe na utaratibu mzuri wa bajeti. Katika mambo ya usimamizi wa matumizi ya Serikali na kazi za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali Rasimu hii ime –“copy” na ku-“paste” Katiba ya sasa bila kutathmini kama mfumo wa hivi sasa unafanya kazi” na kutaka eneo hilo kufanyiwa uchambuzi zaidi.
Aidha alizungumzia haja ya mwongozo wa kudhibiti mikopo na kuongezeka kwa deni la taifa na kusisitiza kuwa uhuru wa serikali zote tatu kukopa ndani na nje ya nchi inaweza kusababisha kukua kwa madeni kupita kiasi.
Aidha alisema kwa kuwa serikali za washirika zina vyanzo vya mapato na Serikali ya Muungano haina, kwa Rasimu ya Katiba hii serikali za washirika ndizo zinazokopesheka na siyo Serikali ya Muungano.
Kuhusu Benki Kuu tatu alisema hakuna haja ya kuwa na hali hiyo kwa kuwa kazi ya Benki Kuu ni kusimamia benki za biashara, sera za fedha na hasa riba, na mfumo wa malipo na kutokaa na hilo kuwa na benki tatu ni kuchochea mgogoro wa kifedha.
“ Moja ya chanzo cha mgogoro wa Euro ni kutokuwepo usimamizi wa pamoja wa benki za biashara. Hivi sasa Ukanda wa Euro unajaribu kuandaa utaratibu wa pamoja wa kuifanya Benki Kuu ya Ulaya (ECB) kusimamia Benki za Biashara.
“ Kama tuna sarafu moja tuwe na Benki Kuu moja. Benki Kuu isiposimamia benki za biashara haitaweza kudhibiti na kusimamia ujazi wa fedha (money supply)” alisema.
Akizungumzia masuala ya Ibara ya 31 inayohusu dini alisema kwamba tatizo la ibara hiyo ni tafsiri ya kukashifu.
“Imani za dini zina tofauti. Imani ya msingi ya dhehebu moja inaweza kuwa kufuru kwa dhehebu lingine na ikatafsiriwa kuwa ni kukashifu. Kuna masuala ambayo jamii inapaswa kujenga maelewano ya kuvumiliana na kuheshimiana na kukubali tofauti za imani bila kugombana. Kuliweka katika Katiba inaweza kujenga chuki na ikatafsiriwa kuwa inalenga kundi fulani.” Alisema Profesa Lipumba na kuuliza kama Ibara ya 5 imelenga kikundi au taasisi ya dini. Je vikundi ambavyo siyo vya dini vinaruhusiwa kukashifu imani na dini? Aliuliza.
Kuhusu vyombo vya ulinzi na usalama alisema kama Serikali ya Muungano ikiwa na Jeshi la ulinzi, Polisi na Usalama wa Taifa huku serikali za washirika zikiruhusiwa kuwa na polisi na usalama wa Taifa, je haitakuwa shida katika utawala hasa ikizingatiwa kwamba ,inawezekana Serikali ya Muungano ikaongozwa na Chama A, Serikali ya Zanzibar ikaongozwa na chama B na Serikali ya Tanzania Bara ikaongozwa na chama C.
“Serikali zote zina polisi na usalama wa taifa wake, haitakuwa kasheshe ndani ya nchi? Sina uhakika Katiba imeweka bayana utaratibu wa kuzuia migongano kati ya vyombo vya Muungano na vyombo vya Washirika”, alisema.
Pamoja na hoja hizo alizotoa Profesa Lipumba kwa niaba ya CUF, aliitaka Tume baada ya kazi kubwa waliyoifanya, wasikubali kuyumbishwa na wahafidhina wasiopenda mabadiliko; akiitaka Tume iwe na msimamo na iangalie wananchi wanataka nini na itetee masuala ya msingi na ya maslahi ya wananchi ambayo inaona ni muhimu yakatetewa kwa maslahi ya Taifa na hasa kwa kuzingatia matakwa ya wananchi.
