OBAMA ABANWA KUMTEMBELEA MZEE MANDELA MAHUTUTI...

Mzee Nelson Mandela.
Ndugu wa karibu wa Rais wa zamani Nelson Mandela na machifu wa familia ya kifalme ya Abathembu jana asubuhi walikutana nyumbani kwake Qunu, Cape Mashariki.

Mmoja wa wanakijiji alisema wengi wao hawakuwa na taarifa za ujio huo hata hivyo walipewa taarifa ya kikao jana asubuhi.
Hatua hiyo ilitokana na mwito wa dharura uliotolewa na watoto wake, wakiongozwa na binti mkubwa, Makaziwe, mwandishi wa Shirika la Habari la Afrika Kusini (SAPA) aliripoti.
Miongoni mwa waliowasili kuhudhuria mkutano huo ni Mandla Mandela,  Thanduxolo Mandela, Ndaba Mandela na Ndileka Mandela. Pia alikuwapo Chifu Bhovulengwe wa Baraza la Kifalme la Abathembu.
Hadi jana saa 4.30 kikao hakikuwa kimeanza. Kilichelewa kwa sababu baadhi ya wanafamilia hawakuwa wamewasili kutokana na kutokuwa na taarifa na jitihada zilikuwa zikifanywa kuwapata.
Napilisi Mandela, ambaye ni mkubwa katika familia ya Mandela, alithibitisha kuwa kikao hicho kitafanyika kama kilivyopangwa.
Alisema kiliitishwa ili kujadili masuala muhimu kuhusu shujaa huyo wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi. Napilisi ndiye kwa kawaida huongoza mikutano na matambiko ya familia hiyo.
Ndugu mwingine wa karibu, Silumko Mandela, alisema mipango ya mwisho kwa ajili ya kikao hicho ilikuwa inaendelea kufanyika.
“Wengi wetu kijijini hapa hatukuwa na taarifa na tuliambiwa leo (jana) asubuhi, hivyo wazee wengi wa familia ya Mandela bado wanahitaji kusafirishwa kuja Qunu kwa ajili ya kikao hicho,” Silumko alisema.
Wakati hayo yakiendelea, maofisa wengi wa Polisi walionekana wametanda katika malango ya kuingilia katika Hospitali ya Medi Clinic alimolazwa Mandela jijini Pretoria.
Kabla ya saa 12 alfajiri, maofisa watatu walionekana katika lango la hospitali hiyo katika barabara yenye watu wengi ya Park.
Maofisa hao walionekana wakipekua magari yanayoingia katika hospitali hiyo ya moyo huku wengine wengi wakiranda ndani ya eneo la hospitali.
Malango mengine yaliyo katika barabara ya Celliers yalifunguliwa kabla ya saa 12 alfajiri huku polisi hao wakishirikiana na walinzi wa hospitali kuyapekua magari yakiwamo yanayobeba wajawazito.
Wananchi wanaomtakia afya njema Mandela, walionekana katika kuta za hospitali hiyo wakiweka kadi, maputo, maua na michoro ya kumtakia afueni ya haraka.
Baadhi ya ujumbe ulioandikwa ukutani ulisomeka: “Wahenga wa (kiongozi wa zamani wa Ghana) Kwame Nkrumah wanakutakia maisha marefu. Bernard (kutoka) Ghana”. Ujumbe mwingine kwenye bendera ya Ethiopia unasomeka: “Tunakupenda baba yetu, Tata Madiba.”
Kadi yenye rangi za kuvutia kutoka shule ya awali ya Montessori imechorwa viganja vya mtoto na picha nyingi za Madiba akiwa amenyanyua Kombe la Dunia la FIFA.
Wanahabari wengi walikusanyika juzi usiku katika hospitali hiyo baada ya Ofisi ya Rais kutangaza kwamba hali ya Mandela imekuwa mbaya. Wengi wao waliondoka eneo hilo juzi saa 9 alfajiri.
Hata hivyo, zaidi ya magari 20 yakiwamo ya kurusha matangazo moja kwa moja kwa ajili ya vituo vya habari vya ndani na nje ya nchi, yalionekana katika barabara ya Celliers juzi asubuhi.
Nyumbani kwa Mandela jijini Johannesburg hali ilikuwa kimya usiku kucha huku asubuhi juzi kukiwa hakuna mtu aliyeonekana akipita. 
Wakati huo huo, ilielezwa kuwa ratiba ya ziara ya Rais Barack Obama wa Marekani haihusishi kiongozi huyo wa Marekani kumtembelea Mandela.
Badala yake atashiriki mazungumzo baina ya nchi mbili hizo, ataongoza mkutano wa mpango wa Viongozi Vijana wa Afrika na kuzuru kisiwa cha Robben, ambako Mandela alifungwa kwa miaka 27, hiyo ni kwa mujibu wa taarifa ya Wizara ya Uhusiano wa Kimataifa iliyotolewa jana. 
Pia atazuru maeneo mbalimbali ya Cape Town na kuhutubia Chuo Kikuu cha Cape Town. “Rais Obama angependa kumwona Mandela,” Waziri wa Uhusiano wa Kimataifa Maite Nkoana-Mashabane aliwaambia waandishi wa habari Pretoria.
“Nchini mwangu, kwa umri wangu na wenu, watu wanapokuwa wanaumwa, huwa tunajaribu kuwapa nafasi ya kupata nafuu,” alisema akimaanisha Mandela.
Kama Obama atakuwa na muda, atatembelea wawakilishi wa Wakfu wa Nelson Mandela, Nkoana-Mashabane alisema. Aliongeza kuwa maisha hayawezi kusimama, kwa sababu Mandela anaumwa.
“Atakatishwa tamaa kama atasikia maisha yamesimama Afrika Kusini (kwa sababu ni mgonjwa).”  Alisema Mandela alikuwa mpiganaji na kila mtu anaendelea kumwombea na kumtakia apone.
Mandela (94) alilazwa hospitalini hapo Juni 8 baada ya kuibuka tena matatizo ya kupumua ambayo yamekuwa yakimkabili kwa muda sasa.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item