ZAIDI YA ASILIMIA 50 YA WABUNGE WAIPITISHA BAJETI YA SERIKALI...

https://roztoday.blogspot.com/2013/06/zaidi-ya-asilimia-50-ya-wabunge.html
![]() |
Dk William Mgimwa. |
Bunge jana lilipitisha Bajeti ya Serikali ya Sh trilioni 18.2 kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura zilizopigwa na wabunge wa Bunge hilo na kuiwezesha Serikali sasa kuanza kazi rasmi Julai mosi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na meza ya Katibu wa Bunge, wabunge waliopiga kura hiyo kwa kuhojiwa mmoja baada ya mwingine, ni 270 kati ya wabunge 354 ambao ndiyo idadi ya jumla ya wabunge hao.
Wabunge waliosema hapana ni wabunge 35 na waliokubali ni wabunge 235 huku wabunge 83 wakiwa hawamo katika ukumbi wa Bunge wakati kura hiyo ikipigwa baada ya wabunge kuitwa kuingia ndani kwa kengele.
Baada ya kura hiyo na matokeo kutangazwa, Spika Anne Makinda alisema sasa Serikali itaanza kazi yake Julai mosi, huku akihimiza fedha zilizopitishwa zifanye kazi iliyokusudiwa ili kuwaletea maendeleo wananchi.
Alisifu Serikali kwa kufanya kazi kubwa kwa kukubali kubadilisha baadhi ya mambo ambayo yalishafikishwa katikati.
Alisema wakati bajeti inajadiliwa ni vema kuzingatia maslahi ya wapiga kura bila kuangalia tofauti za kivyama ndani ya Bunge hilo.
Mapema akifanya majumuisho, Waziri wa Fedha, Dk William Mgimwa, alipongeza wabunge waliochangia na kuahidi kuwa hoja zao zimefanyiwa kazi na Serikali na hivi punde wakati wa kujadili sheria ya fedha zitatolewa majibu.
Baadhi ya hoja hizo ni za kupunguza kodi katika baadhi ya maeneo na pia kuangalia upya mapendekezo ya kupunguza kodi kwenye pikipiki za biashara-bodaboda, simu za mkononi ambazo pia zimekuwa zikitumiwa kutuma fedha. Hata hivyo alisema Bajeti yake inajielekeza zaidi vijijini.
Akijenga hoja kwa nini ni bajeti ya vijijini, Mgimwa alisema anataka wananchi vijijini wanufaike kwa kutoa kipaumbele katika mahitaji ya wananchi hao.
Mahitaji ya umeme vijijini yameongezwa fedha zaidi kwa mujibu wa Mgimwa, ambapo sasa Mamlaka ya Umeme Vijijini (REA), iliyokuwa imepangiwa Sh bilioni 153 katika bajeti ya awali, imeongezwa Sh bilioni 186, ili ipeleke umeme vijijini.
Katika sekta ya maji, alisema Serikali imekubali kuongeza Sh bilioni 184, sekta ya miundombinu ya usafirishaji ikiongezwa Sh bilioni 30 huku Maeneo Maalumu ya Uwekezaji (EPZ), yakiongezwa Sh bilioni 30, ili kukuza uwekezaji na sekta ya mifugo ikiongezwa Sh bilioni 20.
Tofauti na ilivyotarajiwa na wengi, kwamba Waziri Mgimwa, angefafanua kama amepunguza kodi au la katika maeneo yaliyotarajiwa zaidi kama mafuta jamii ya petroli, Waziri aliwataka wabunge wasubiri ufafanuzi.
Hoja zilizotakiwa kusubiri ufafanuzi wakati Muswada wa Sheria ya Fedha utakapoletwa keshokutwa, bila kufafanua kama zimekubaliwa kama wabunge walivyoomba au la, ni pamoja na ombi la punguzo la kodi ya mshahara la asilimia moja, kuongezwa hadi asilimia 3.
Nyingine ni kodi katika petroli na dizeli, ambayo ilipendekezwa na Kamati ya Bajeti na baadhi ya wabunge kwamba kusiwepo nyongeza ya aina yoyote ya kodi katika bidhaa hizo.
Katika Bajeti ya Serikali, ilipendekezwa kuwa ushuru katika mafuta ya dizeli uongezwe kwa Sh 2 kwa kila lita kutoka Sh 215 inayotozwa sasa mpaka Sh 217.
Katika petroli, Serikali ilikusudia kuongeza ushuru wa Sh 61 kwa kila lita, kutoka Sh 339 inayotozwa sasa kwa kila lita, mpaka Sh 400 kwa lita.
Mgimwa katika majibu yake ya jana, hakusema kama amekubaliana na wazo hilo la Kamati ya Bajeti na baadhi ya wabunge, badala yake alisema amelishughulikia na atafafanua zaidi wakati wa Muswada wa Sheria ya Fedha.
Hata hivyo, alifafanua kuwa kazi iliyofanyika katika mafuta ya petroli, imezingatia kuzuia uchakachuaji, jambo linaloonesha, ushuru wa mafuta ya taa yaliyokuwa yakitumika kuchakachua dizeli, hautashuka.
Kuhusu kodi ya mshahara, Mgimwa alitoa historia ya kupunguza kodi hiyo kuanzia mwaka 2007/08 ilipokuwa asilimia 18.5 katika kima cha chini mpaka asilimia 14 mwaka huu wa fedha na sasa kusudio ni kupunguza kwa asilimia moja mpaka 13.
Kamati ya Bajeti, ilitaka ipungue kwa asilimia tatu mpaka 10 lakini Mgimwa alisema Serikali itaendelea kutafuta namna ya kupunguza kodi hiyo.
Kuhusu mapendekezo ya Serikali kuongeza ushuru katika huduma zote za simu kutoka asilimia 12 ya sasa hadi 14.5 kwa mwaka ujao wa fedha, Kamati ya Bunge ilishauri nyongeza ya asilimia 2.5 ifutwe, lakini Mgimwa alisema, atafafanua katika Sheria ya Fedha.
Katika ushuru wa bodaboda wa barabara, ambao Serikali ilitaka kuusamehe na wabunge kupinga kwa maelezo kwamba watakaofaidika si vijana wanaoziendesha wanaolengwa, bali wamiliki wa usafiri huo, Mgimwa alisema amelifanyia kazi na itaonekana katika Sheria ya Fedha, baada ya kuupata ukweli kutoka kwa vijana hao.
Wakati huo huo Chadema, ilitoa taarifa jana kuwa imegoma kuhudhuria kikao cha kupitisha Bajeti kwa madai kwamba, Bunge haliwajali, halikusitisha shughuli zake kuomboleza, wala halikutoa hata pole. Pia walidai walinyimwa kusoma maoni yao, kwa kuwa awali bajeti ilitakiwa kupitishwa leo, badala ya jana.
Wakati wabunge wa Chadema walipokuwa wakiitwa kukubali au kukataa bajeti, wabunge wa CCM walifungua vipaza sauti na kusema “maandamano”.