TAKUKURU YAOKOA SHILINGI BILIONI 3.2 ZA SERIKALI KWENYE MALIPO 'FEKI'...

https://roztoday.blogspot.com/2013/06/takukuru-yaokoa-shilingi-bilioni-32-za.html
![]() |
George Mkuchika. |
Serikali imefanikiwa kuokoa jumla ya Sh.bilioni 3.2 kutokana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) kusimamisha malipo baada ya kuonekana kuwa si halali.
Hayo yalisemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Utawala Bora), George Mkuchika juzi alipokuwa akitoa neno la shukrani kwenye sherehe ya kuwaaga viongozi na watumishi wa Tamisemi, waliohama na kustaafu.
Mawaziri waliohama Ofisi ya Waziri Mkuu Tamisemi ni Celina Kombani ambaye sasa amehamishiwa Ofisi ya Rais Utumishi na George Mkuchika ambaye alitoka Ofisi ya waziri Mkuu Tamisemi kwenda Waziri wa Nchi Ofisi ya rais Ikulu.
Wengine walioagwa na kupongezwa ni makatibu wakuu waliohama ofisi wa waziri mkuu, Makatibu tawala wa Mikoa na wakurugenzi wa mamlaka za serikali za mitaa waliostaafu, watumishi waliostaafu ofisi ya Waziri Mkuu na watumishi waliohama
Jumla ya watumishi waliotakiwa kutunukiwa zawadi walikuwa 59 lakini waliohudhuria sherehe hizo walikuwa 35 ambapo zawadi mbalimbali zilitolewa ikiwemo, seti za televisheni, picha kubwa za ukutani za nyumba za asili, na zawadi nyingine.
Akizungumza Waziri Mkuchika alisema ipo kero ya rushwa na wizi katika halmashauri mbalimbali nchini na wakati mwingine wafanyakazi wa wizara wanashirikiana na watendaji wa halmashauri kufanya vitendo hivyo viovu.
Mkuchika alisema kwamba fedha hizo zilizookolewa zilikuwa zinapotea kutokana na kuwapo kwa rushwa katika shughuli zilizofanywa na halmashauri mbalimbali.
Kutokana na tatizo hilo Mkuchika amewataka Watendaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kujiepusha na rushwa kwani kumekuwa na vitendo vya wafanyakazi wa wizara kushirikiana na watendaji wa halmashauri katika wizi huo.
Alisema sasa kazi aliyopewa ni kuangalia halmashauri zinavyokwenda na kuwataka watendaji kushikilia rekodi ya hati safi kwenye halmashauri na kujiepusha na vitendo vya rushwa ambavyo vimekuwa vikifanywa na watu wa Wizarani na halmashauri.
“Wizara niliyohamia inajishughulisha na kupambana na rushwa isije ikawa umepita huko mambo yakawa mabaya ukaja Mzee naomba nisaidie kwa hilo sitakuwa na msaada kila mtu analinda kitumbua chake” alisema.
Mkuchika alisema tangu mkaguzi mkuu alipoanza kukagua vitabu vya halmashauri nusu ya hati zilikuwa chafu lakini katika ukaguzi wa mwaka jana kuna hati moja tu ambayo ilitokana na kula njama kati ya mtumishi wa halmashauri na mtumishi wa Wizarani.
“Mara chache mtu kusimama na kuipongeza Tamisemi, kuna halmashauri zaidi ya 130 nchini na kupatikana hati chafu moja tu ni mafanikio makubwa katika utendaji” alisema
Alisema ni lazima ukifanya kazi Tamisemi ukubali lawama kwani ni wizara inayojishughulisha na watu na maisha ya watu hivyo uadilifu ni jambo linalotakiwa ili kuweza kuondoa malalamiko katika wizara hiyo.
Mkuchika ambaye alipewa zawadi ya televisheni ya inchi 32 na picha ya ukutani, alimpongeza Waziri Mkuu kwa zawadi hiyo kwani televisheni yake aliyokuwa ameiweka chumbani kwake iliungua mwezi mmoja uliopita.
“Nashukuru sana kwa zawadi hii lazima niseme ukwei TV niliyokuwa nimeweka chumbani ambayo ilikuwa ikinipa fursa ya kuangalia mapitio ya magazeti kila asubuhi ilikuwa imeungua kama mlijua hitaji langu” alisema
Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa Mstaafu, Getrude Mpaka alisema alitaka serikali kuweka msisitizo wa kozi za wastaafu ili waweze kujiandaa na pia serikali iwaandae wastaafu kuwa na gari na nyumba.
Akizungumza katika sherehe hizo, Waziri Mkuu Mizengo Pinda, alisema hiyo ni fursa nzuri ya kubadilishana mawazo kwa wale waliostaafu na kutakiana kila la kheri kwa wale ambao wamehamishiwa kwenye taasisi nyingine.
Alisema kufanya kazi kipindi chote hadi kustaafu salama ni jambo jema kutokana na utumishi wa umma kuwa na changamoto nyingi .
“Waulizeni wastaafu mara ngapi wamesingiziwa mambo ya ovyo huyo Chadema au huyo CUF na anayesema hivyo utadhani ni msafi sana.” Alisema
Alisema wale waliohamishiwa maeneo mengine serikali imeona utendaji wenu kuwa mnaweza kuleta mabadiliko kwenye taasisi na maeneo mapya mliyopangiwa.
Waziri Mkuu alisema Chama cha Wafanyakazi (TUCTA), wameanzisha wazo ambalo ni zuri la kuandaa watumishi kustaafu na mtumishi anapofanya kazi kwa audilifu lazima apongezwe.