WANAFUNZI SHULE ZA MSINGI WALISHWA MIHADARATI KWENYE BARAFU...

Mojawapo ya aina za mihadarati.
Baadhi za chakula ikiwamo mikate na barafu zinazouzwa kwenye shule za msingi zinadaiwa kuwekwa dawa za kulevya hali inayosababisha watoto kuathirika.

Hayo yalisemwa jana katika taarifa iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, William Lukuvi kwenye kilele cha maadhimisho ya kitaifa ya siku ya kupinga dawa za kulevya duniani.
Lukuvi ambaye alimwakilisha Waziri Mkuu, Mizengo Pinda katika maadhimisho hayo yaliyofanyika hapa, alisema Serikali itaanza kufuatilia  biashara hizo shuleni.
Alisema, “sasa dawa hizi zinauzwa hadi kwenye vitu ambavyo watoto wanakula katika shule za msingi, kwa mfano hivi sasa dawa hizo zinawekwa kwenye maandazi, mikate na barafu.
“Ni lazima kufahamu watu gani wanauza vyakula vya aina hiyo na wana nia gani,” alisema Lukuvi.
Kwa mujibu wa Lukuvi, watu hao wanafanya jambo ambalo limekuwa likifanya vijana wengi wa shule za msingi na hata sekondari kuwa na tabia za ajabu.
Alisema  kutokana na hali hiyo, mtoto wa shule anaingia darasani akiwa na kiatu kimoja mguuni, mkufu wenye nyembe, kidani chenye nyembe kifuani, wanaingia na misumari mifukoni , hawafungi lisani za suruali zao na wengine kutembea vifua wazi, jambo ambalo alisema Serikali lazima iliangalie.
Hata hivyo, Lukuvi alisema vita dhidi ya dawa za kulevya bado ni kubwa kutokana na wanaoendesha biashara hizo kuwa na fedha za kutoa rushwa na kuhonga kwa lengo la kuzuia kukamatwa au kutofikishwa katika vyombo vya Dola.
Waziri Lukuvi alisema vita hiyo si kubwa kwa Tanzania pekee, kwani wanaofanya biashara hiyo ni wenye fedha nyingi na uwezo mkubwa. Alisema kwa Tanzania wanajitahidi kukamata dawa hizo na kuwa mfano kwa nchi za Afrika zinazoizunguka.
Alisema kuanzia mwaka  2008  hadi  mwaka jana,  watuhumiwa  10,799 walikamatwa  wakijihusisha na  dawa hizo nchini. Watanzania wapatao 240 walikamatwa Brazil, Pakistani na Afrika Kusini  wakijihusisha na masuala hayo.
Alisema hali hiyo inaharibu taswira ya nchi na kusababisha  Watanzania wasio na  hatia  kupata  usumbufu na masharti  magumu  kwa Watanzania wanapotaka kusafiri  kwenda nchi zingine kutokana na  sifa mbaya  inayojengeka.
Alisisitiza kuwa kwa bahati mbaya  hivi sasa rika la watumiaji wa dawa  hizo ni vijana  wa shule  za msingi hadi vyuo.
Alisema watumiaji hao ndio wazururaji, waporaji, wakabaji na wabakaji mitaani, lakini ndio pia omba omba  mitaani na mwisho hukumbwa na magonjwa ya akili, Ukimwi na hatimaye kifo.
Kamishna  wa Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya Tanzania, Christopher Shekiondo, alisema wamekuwa wakipambana na tatizo hilo  kwa  nguvu kubwa, na kufanikiwa kukamata wahalifu wa kimataifa wanaotafutwa duniani na kesi zinaendelea mahakamani.
Alisema changamoto kubwa ni wimbi kubwa la watumiaji wa dawa hizo kutokana na wengi hivi sasa kuwa ni watoto wadogo wa shule za msingi hadi vyuo vikuu.
Aliongeza kuwa wafanyabishara hao wamekuwa wakitumia mbinu nyingi za kuziingiza nchini  na kushawishi  vijana  kuzitumia, jambo ambalo alisema ipo haja kubwa ya kuwepo ushirikiano kati ya Serikali na jamii.
Juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari, Lukuvi alisema  katika kipindi cha miaka mitatu tangu 2010 hadi Mei mwaka huu, kilo 742.5 za heroin,  348.3 za cocaine na kilo 77,740 za bangi zilikamatwa na ekari 284 za mashamba ya bangi zimeteketezwa.
Alisema takwimu za tiba kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii  zinaonesha watumiaji waliofika katika vituo vya tiba nchini kupata huduma za tiba katika kipindi cha 2008 hadi 2011 walikuwa 20,626.
Pia watumiaji zaidi ya 800 wa dawa za kulevya aina ya heroin wanaendelea kupata tiba katika vituo vya Muhimbili na Mwananyamala jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia mapambano dhidi ya  dawa hizo, alisema jitihada zimefanyika kuzuia kilimo cha bangi, uingizaji na usambazaji wa dawa hizo.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item