YA HOSNI MUBARAK, SASA YAMKUMBA MORSI NCHINI MISRI...
https://roztoday.blogspot.com/2013/07/ya-hosni-mubarak-sasa-yamkumba-morsi.html
![]() |
| KUSHOTO: Mohammed Morsi. KULIA: Hosni Mubarak. |
Jaji Mkuu wa Mahakama ya Katiba, Adly Mahmud Mansour, ameapishwa rasmi kuwa Rais wa muda siku moja baada ya Jeshi kumng'oa madarakani Rais Mohammed Morsi na kumweka kizuizini nyumbani kwake.
Baada ya kuapishwa jana, Mansour alisema uchaguzi mpya ndiyo njia bora ya kufuata katika mustakabali mwema wa nchi, lakini hakutamka ni lini utafanywa.
Morsi ambaye alikuwa Rais wa kwanza kuchaguliwa kwa njia ya sanduku la kura, yuko kizuizini nyumbani kwa alichokisema ni mapinduzi ya kijeshi yaliyofanyika dhidi yake. Lakini Jeshi lilisema "alishindwa kukidhi mahitaji ya watu."
Hatua hiyo ya kumwondoa ilifika baada ya siku kadhaa za maandamano na mikutano dhidi yake na chama chake cha Muslim Brotherhood.
Waandamanaji walimtuhumu kwa kuendekeza ajenda ya Uislamu na kushindwa kukabiliana na matatizo ya kiuchumi yanayoikabili nchi.
Mansour alisema ni heshima kwake kupokea amri ya kutwaa madaraka wakati huu wa kipindi cha mpito. Aliwapongeza vijana na wanajeshi ambao alisema wamekuwa "roho ya Taifa na usalama wa nchi."
Mkuu wa Majeshi Jenerali Abdul Fattah Al-Sisi, alionekana kwenye televisheni akitangaza rasmi kusimamishwa kwa Katiba ya nchi huku amezungukwa na viongozi wa kijeshi na kidini na kusema kuwa Jaji Mkuu wa Mahakama ya Katiba ndiye atakabidhiwa madaraka ya urais.
Wakizungumzia hatua hiyo viongozi mbalimbali wa nchi na Serikali walitoa maoni yao:
Rais Barack Obama wa Marekani alisema, "tumesikitishwa sana na uamuzi wa Jeshi la Misri kumwondoa Rais Morsi na kusimamisha Katiba ya nchi. Sasa nalitaka Jeshi la Misri kuharakisha kurejea katika utawala wa kidemokrasia kwa kuchagua Serikali ya kiraia kupitia mchakato shirikishi na wa uwazi, na iepuke kumkamata Rais Morsi na wafuasi wake.
"Kutokana na nilichoambiwa leo (jana), nimeelekeza pia idara husika na mashirika kuangalia athari za hatua hiyo chini ya Sheria ya Marekani, kuhusu misaada yetu kwa Serikali ya Misri," alisema Obama na kuongeza kuwa sauti za waliopinga kwa amani zinapaswa kusikilizwa-ikiwa ni pamoja na wanaounga mkono hatua ya mapinduzi, na waliokuwa wakimwunga mkono Morsi.
Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron alisema: "Hatuungi mkono majeshi kuingilia Serikali, lakini tunachohitaji kifanyike Misri sasa ni demokrasi kutamalaki na kuleta mabadiliko ya kidemokrasia. Pande zote zinatakiwa kushirikishwa katika hilo, na ndicho Uingereza na washirika wake wanawaambia Wamisri kwa uwazi."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Guido Westerwelle alisema: "Hili ni anguko la demokrasia nchini Misri. Misri haina budi sasa kuharakisha kurudi katika kuheshimu Katiba. Kuna hatari kwamba mabadiliko ya kidemokraia Misri yatakuwa yametibuliwa."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergey Lavrov alisema: "Tunadhani kwamba ni muhimu sasa kwa vikundi vyote vya kisiasa kuonesha kuvumiliana kufikiria maslahi mapana ya kitaifa yatokanayo na vitendo vyao, na kuthibitisha kuwa wanadhamiria kutatua matatizo yaliyopo ya kisiasa na kiuchumi katika utaratibu wa kidemokrasia, bila ghasia na kujali maslahi ya vikundi vyote vya kijamii na kidini."
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Ban Ki-moon alisema: "Kwa kipindi hiki ambacho kuna mvutano mkubwa na kukosekana kwa uhakika wa mustakabali wa nchi, nasisitiza mwito wa utulivu na kuacha ghasia, kufanya majadiliano bila kuzuiana.
Alisema utaratibu wa kushirikishana ni muhimu katika kushughulikia mahitaji na matatizo ya Wamisri wote. Kuheshimu haki za msingi, ikiwa ni pamoja na uhuru wa kujieleza na kukusanyika.
Aliongeza kuwa katika maandamano yaliyofanywa, Wamisri walitoa sauti halali za matatizo yanayowakabili, na kuonya kwamba kuingilia kati na Jeshi katika masuala ya Taifa lolote ni jambo lisilokubalika.
"Hivyo litakuwa jambo la maana kurejesha utawala wa kiraia haraka iwezekanavyo kwa mujibu wa kanuni za kidemokrasia," alisema Ban.
Mkuu wa Sera za Nje za Umoja wa Ulaya, Catherine Ashton alisema: "Nazitaka pande zote kurudi haraka kwenye mchakato wa kidemokrasia, ikiwa ni pamoja na kufanya uchaguzi huru na wa haki wa Rais na Bunge na kuidhinisha Katiba, kwa kushirikisha wadau wote, ili kuruhusu nchi kuanza na kukamilisha mageuzi ya kidemokrasia.
"Natumani utawala mpya utashirikishwa kikamilifu na nasisitiza umuhimu wa kuhakikisha heshima ya haki za binadamu, uhuru na utawala wa sheria na mamlaka husika ziwajibike kwa hili," alisema.
Alilaani vitendo vya ghasia na kutoa salamu za pole kwa familia za waliopoteza maisha na kutaka vikosi vya usalama kufanya kila linalowezekana, kulinda maisha na ustawi wa wananchi wa Misri. "Natoa mwito kwa pande zote kuhakikisha haki inatendeka."
Mfalme Abdullah wa Saudia, alisema: "Katika jina la watu wa Saudi Arabia na kwa niaba yangu, tunaupongeza uongozi wako wa Misri katika kipindi hiki kigumu katika historia ya nchi.
"Tunamwomba Mungu akusaidieni kutumia madaraka mliyonayo kutimiza matamanio ya ndugu zetu wa Misri."
Mbunge wa Gaza (Hamas), Yahia Moussa, alisema chama cha Hamas hakiwezi kuingilia mambo ya ndani ya Misri, hivyo hakina cha kusema juu ya uamuzi wa Jeshi la Misri kumwondoa Rais Morsi.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), Abdullah bin Zayed al-Nahayan, alielezea imani yake kwa watu wa Misri kwamba wana uwezo wa kuvuka kipindi hiki cha matatizo ambamo Misri imekuwa ikipita.
Shekhe Abdullah alisema Jeshi la Misri lina uwezo wa kuthibitisha tena kwamba ndilo uzio wa Misri na kwamba ndilo mlinzi na ngao imara ambayo inahakikisha kwamba Misri inabaki kuwa Taifa linaloheshimu Katiba na sheria."
Rais Bashar al-Assad wa Syria, alisema: "Kinachotokea Misri ni kuanguka kwa kile kinachoitwa Uislamu wa kisiasa. Huo ndio mwisho wa kila mtu anayejaribu kutumia dini kwa maslahi ya kisiasa au vikundi."
Wizara ya Afya ilisema takriban watu 10 waliuawa na wengi kujeruhiwa katika mapambano ya pande zinazopingana nchini yaliyotokea usiku wa kuamkia jana. Watu wapatao 50 walipoteza maisha tangu kuanza kwa machafuko hayo Jumapili.
Morsi alipanda ngazi ndani ya chama ambacho kilipigwa marufuku miongo kadhaa huko nyuma, akafikia kuwa Mwenyekiti wa tawi la kisiasa, la The Freedom and Justice.
Kwa ushindi finyu wa urais Juni mwaka jana, aliibuka kuwa Rais wa kwanza kuchaguliwa kidemokrasia. Uchaguzi huo, ambao ulionekana kwa jumla kuwa huru na wa haki, ulifanyika baada ya kipindi cha ghasia chini ya utawala wa kijeshi, alipopinduliwa Rais Hosni Mubarak Februari 2011.
Rais Mubarak, ambaye aliongoza nchi hii kwa takriban miaka 30 alilazimishwa kuachia madaraka kwa maandamano makubwa. Waandamanaji walisema walishachoshwa na kiwango kikubwa cha umasikini, rushwa na ukosefu wa ajira katika nchi hii kubwa kuliko zote ya kiarabu.
Katika kipindi cha madaraka ya Morsi, alishindwa kuelewana na taasisi muhimu na sekta za kijamii, na kuonekana na Wamisri wengi kama kiongozi asiyefanya kikubwa kukabiliana na matatizo ya kiuchumi na kijamii.
Misri ikagubikwa zaidi na ufa kati ya wafuasi wa kiislamu wa Morsi na wapinzani wao, wakiwamo wenye mrengo wa kushoto, wa kati na wa kidini.
Juni 30, mamilioni ya wananchi waliingia mitaani kuadhimisha mwaka mmoja wa Morsi madarakani, katika maandamano yaliyopangwa na wafuasi wa chama cha Tamarod (waasi).
Maandamano hayo yalilifanya Jeshi kumwonya Morsi Julai mosi, kwamba litaingilia kati na kuja na mipango yake kama atashindwa kukidhi mahitaji ya umma katika saa 48.
Wakati kipindi alichopewa kikikaribia kumalizika, Morsi akasisitiza kwamba yeye ni kiongozi halali wa Misri. Akaonya kwamba juhudi zozote za kumng'oa zitaiingiza nchi katika machafuko.
Baada ya kuonekana hakuna suluhisho lolote la kisiasa huku vifo vikiongezeka kutokana na ghasia hizo na amani ikiendelea kuvunjika, Jeshi lilitwaa madaraka ili kuepusha nchi kuingia katika machafuko zaidi.
Jeshi hilo ni chombo chenye nguvu zaidi serikalini na wengi wanasema linaendesha mambo yake kama serikali ndani ya serikali. Biashara zinazoendeshwa na Jeshi hilo ni sehemu muhimu katika kuchangia pato la Taifa la Misri.
