HATIMAYE MIILI YA WATOTO WA MANDELA YAFUKULIWA NA KUREJESHWA QUNU...
https://roztoday.blogspot.com/2013/07/hatimaye-miili-ya-watoto-wa-mandela.html
![]() |
| Maofisa wa polisi wakibeba jeneza lenye mabaki ya miili ya watoto wa Nelson Mandela jana. |
Hatimaye mabaki ya miili ya watoto watatu wa Rais mstaafu wa Afrika Kusini, Nelson Mandela, kikiwamo kichanga kilichofariki dunia mwaka 1948, yamefukuliwa katika makaburi ya Mvezo, alikozaliwa shujaa huyo wa vita dhidi ya ubaguzi wa rangi duniani.
Hatua hiyo ya juzi ilitanguliwa na mgogoro katika familia ya Mandela, uliotokana na mabishano kuhusu wapi anapaswa kuzikwa kiongozi huyo, kati ya Mvezo alikozaliwa na Qunu alikokulia.
Pia imekiuka ushauri wa Kaimu Mwenyekiti wa Kabila la Abathembu, linalozungumza lugha ya Xosa, Inkosi Tanduxolo Mtirara, aliyeonya kuwa mila na desturi za kabila hilo na makabila mengi ya Afrika, zinakiukwa kwa kujadili maziko ya mtu aliye hai.
"Hakuna kufukua miili wala kuandaa makaburi. Hakuna mtu anayeruhusiwa kutembelea kaburi la mtu aliye hai.
"Hii ni mara ya kwanza imetokea katika familia yetu na kama tutashindwa kumaliza mgogoro huu, tunaingia katika hatari ya kusababisha utamaduni, miiko na mila zetu, zidharauliwe na dunia," alionya Mtirara mwanzoni mwa wiki hii.
Awali, Mandela ambaye leo anatimiza siku 28 akiwa katika Hospitali ya Medi-Clinic, Pretoria akipumulia mashine baada ya kuugua mapafu, kwa kauli yake alitaka azikwe karibu na makaburi ya wanawe bila kutaja eneo, ingawa wosia wake unataka yeye azikwe Qunu.
Wanawe hao, Makgato aliyefariki dunia mwaka 2005; Makaziwe, ambaye ni mwanawe wa kike wa kwanza aliyefariki dunia akiwa mchanga na Madiba Thembekilea, aliyekufa kwa ajali ya gari mwaka 1969; walizikwa Qunu, lakini Mandla alifukua miili yao mwaka 2011 na kuizika upya Mvezo, alikozaliwa babu yake.
Mandla ambaye ni Mbunge wa ANC ni mtoto wa Makgato, kiongozi mkuu wa ukoo wa Madiba, anaotoka Mandela.
Pamoja na wadhifa wake, uamuzi wa Mandla ambao haukushirikisha familia, ulisababisha watoto wa Mandela, wakiwakilishwa na Mwanasheria, Sandla Zigadla, kwenda mahakamani kutaka mabaki ya ndugu zao, yarudishwe Qunu.
Jaji Lusindiso Pakade, alitoa amri ya muda Ijumaa iliyopita, akimwamuru Mandla kuacha kuingilia mchakato wa kuhamisha mabaki ya miili hiyo kutoka Mvezo.
Juzi Jaji Pakade, alikataa jaribio la Mandla kutaka kuzuia utaratibu wa kufukua miili hiyo na kurudishwa Qunu, ilikokuwa imezikwa tangu awali na badala yake akakazia hukumu kwa amri ya Mahakama, ikitaka miili hiyo ifukuliwe haraka.
Baada ya kuifukua jana uchunguzi wa kisayansi wa kuthibitisha kwamba ni miili ya watoto hao ulifanyika na kuzikwa upya Qunu jana.
Hata hivyo, Msemaji wa Mandla, alisema Chifu huyo wa Mvezo, alitarajiwa kukutana na waandishi wa habari baadaye jana, kutoa taarifa ya hatua atakazochukua.
