RAIS KIKWETE AWAPANGUA MAKATIBU WAKUU WA WIZARA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/08/rais-kikwete-awapangua-makatibu-wakuu.html
Ombeni Sefue. |
Rais Jakaya Kikwete amefanya mabadiliko ya makatibu wakuu wa wizara na naibu wao, kwa kupandisha cheo naibu katibu wakuu wengi, kuwa makatibu wakuu, kuteua wapya, kuwabadilisha wizara na wengine kusubiri kupangiwa kazi maalumu.
Akizungumza jana Dar es Salaam, Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, alisema mabadiliko hayo ni jitihada za Rais kuimarisha na kuboresha ufanisi katika utendaji wa shughuli za Serikali.
Katika mabadiliko hayo, Rais Kikwete aliyeondoka jana kwenda Zimbabwe kuhudhuria sherehe za kuapishwa kwa Rais Robert Mugabe, ameteua Katibu Mkuu wa Tume ya Vyuo Vikuu (TCU), Profesa Sifuni Mchome kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Naibu katibu wakuu walioteuliwa na kuwa makatibu wakuu, ni pamoja na Jumanne Sagini aliyekuwa Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ambapo sasa ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo.
Pia, Dk Servacius Likwelile aliyekuwa Wizara ya Fedha, sasa amekuwa Katibu Mkuu katika wizara hiyo.
Naibu katibu wakuu wengine waliopandishwa na kuwa katibu wakuu ni Alphayo Kidata aliyekuwa Tamisemi, ambaye sasa anakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Dk Patrick Makungu aliyekuwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, sasa amekuwa Katibu Mkuu wizara hiyo.
Wengine ni Dk Shaaban Mwinjaka aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ambaye sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Uchukuzi na Uledi Mussa aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, sasa ni Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko.
Aidha Sefue alisema aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Charles Pallangyo, ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, kuziba nafasi iliyoachwa wazi na aliyekuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Blandina Nyoni aliyesimamishwa kutokana na mgomo wa madaktari.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Anna Maembe ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana na Utamaduni, Sihaba Nkinga naye ameteuliwa kuwa Katiba Mkuu wa wizara hiyo na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Sophia Kaduma ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu wizara hiyo pia.
Aidha Balozi Sefue alisema Rais Kikwete katika mabadiliko hayo amehamisha baadhi ya makatibu wakuu, ambapo Dk Florence Turuka aliyekuwa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia amekuwa Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko, Joyce Mapunjo, sasa atakuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, kuchukua nafasi ya Dk Stergomena Tax, ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC).
Katika mabadiliko ya naibu katibu wakuu, Balozi Sefue alisema Rais Kikwete ameteua naibu katibu wakuu wapya ambao ni Angelina Madete aliyekuwa Msaidizi wa Katibu wa Baraza la Mawaziri Ikulu, ambaye anakwenda Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.
Wengine ni Regina Kikuli aliyekuwa Kaimu Katibu Mkuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu na Zuberi Samataba aliyekuwa Mkurugenzi wa Elimu ya Shule za Msingi, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, anakuwa Naibu Katibu Mkuu Tamisemi-Elimu.
Naibu makatibu wengine wapya ni Edwin Kiliba aliyekuwa Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, ambaye anakuwa Naibu Katibu Mkuu Tamisemi na Dk Deodatus Mtasiwa, aliyekuwa Mganga Mkuu ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu Tamisemi-Afya, ambayo ni nafasi mpya iliyoongezwa.
Aidha Sefue alisema naibu makatibu wakuu wengine ni Dk Yamungu Kayandabila, aliyekuwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Kodi, anakwenda Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Profesa Adolf Mkenda aliyekuwa Mkuu wa Idara ya Uchumi, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam anakwenda Wizara ya Fedha-Sera na Dorothy Mwanyika, aliyekuwa Katibu Tawala Mwanza, anakwenda Wizara ya Fedha-Fedha za Nje na Madeni.
Wengine ni Rose Shelukindo, aliyekuwa Mkurugenzi wa Utawala Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki, anakuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Selassie Mayunga aliyekuwa Idara ya Ramani Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi, anakuwa Naibu Katibu Mkuu wizarani hapo.
Aidha Mponica Mwamunyange, aliyekuwa Kamishna wa Bajeti Wizara ya Fedha anakwenda Wizara ya Uchukuzi kuwa Naibu Katibu Mkuu.
Pamoja na hao, Balozi Sefue aliwataja naibu katibu wakuu wengine kuwa ni Consolata Mgimba, anayekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Profesa Elisante Laizer aliyekuwa Mkurugenzi wa Vijana Wizara ya Habari, anakuwa Naibu Katibu Mkuu wizarani hapo na Armnantius Msole, anayekwenda Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
Balozi Sefue pia alisema katika mabadiliko hayo, naibu makatibu wakuu waliohamishwa wizara ni pamoja na John Mngodo, anayetoka Wizara ya Uchukuzi kwenda Wizara ya Mawasiliano na Selestine Gesimba, anayetoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kwenda Wizara ya Maliasili na Utalii.
Wengine ni Ngosi Mwihava anayetoka Ofisi ya Makamu wa Rais na kuhamia Wizara ya Nishati na Madini ikiwa ni nafasi mpya ambayo awali haikuwepo, na Maria Bilia anayetokea Wizara ya Ardhi Nyumba na Makazi na kuhamishiwa Wizara ya Viwanda na Biashara. Nuru Milao ametolewa Wizara ya Maliasili na Utalii na kuhamishiwa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto.
Kwa mujibu Sefue katika mabadiliko hayo yaliyofanywa na Rais Kikwete aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana na Michezo, Sethi Kamuhanda, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Kijazi Mtengwa na aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchukuzi, Omari Chambo watapangiwa kazi nyingine.
Alisema katika uteuzi huo, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Peniel Lyimo, amehamishiwa Ofisi ya Rais Ikulu, kwenye Taasisi ya Kumsaidia Rais Kusimamia Utekelezaji wa Masuala mbalimbali ambapo katika taasisi hiyo, atakuwa Naibu Mtendaji Mkuu atakayeanzisha na kuongoza Idara ya Mageuzi ya Kilimo.
Kwa upande wa wanaostaafu, aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Patrick Rutabanzibwa amestaafu mwenyewe kwa hiari yake.
Akizungumzia mabadiliko hayo, Sefue alisema lengo la Rais Kikwete ni kuimarisha utendaji ndani ya Serikali.
Aidha kuhusu hatma ya waliokuwa makatibu wakuu Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Blandina Nyoni na wa Nishati na Madini, David Jairo, Balozi Sefue ataweka hadharani uchunguzi wa tuhuma dhidi yao utakapokamilika na kwa upande wa Dk Mtasiwa, tayari Rais Kikwete amejiridhisha kuwa hakustahili kuadhibiwa.