WAZIRI MWAKYEMBE HATISHIKI NA KUJITOA KWA RWANDA
https://roztoday.blogspot.com/2013/08/waziri-mwakyembe-hatishiki-na-kujitoa.html
- Asema nchi haitayumba,aahidi kuondoa vizuizi 56 & marekebisho ya miundombinu
MSIKU MOJA baada yabaada ya Rwanda kutangaza kutotumia Bandari ya Dar es Salaam, kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu kupitisha mizigo ya wafanyabiashara wake,Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, ametupilia mbali madai ya Serikali ya Rwanda kwamba itaacha kutumia Bandari ya Dar es Salaam, kwa ajili ya kusafirisha mizigo yake.
Kutokana na hali hiyo, Dk. Mwakyembe amesema Tanzania haiwezi kuyumbishwa, badala yake inajikita zaidi kuimarisha sekta ya uchukuzi.
Akifungua semina ya wadau wa sekta ya Usafirishaji mjini Dar es Salaam jana, Dk. Mwakyembe alisema haamini kama Rwanda wanaweza kujitoa kupitisha mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam, kwa sababu wamekuwa na unafuu wa kufupisha safari zao.
Dk. Mwakyembe, alitoa kauli hiyo, kufuatia tamko la nchi mbili za Rwanda na Uganda kutangaza kutotumia Bandari ya Dar es Salaam, kuanzia Septemba Mosi, mwaka huu katika kupitisha mizigo ya wafanyabiashara wake.
Uamuzi huo, ulibainika baada ya Umoja wa Wasafirishaji wa Mizigo kwa njia ya Barabara Tanzania (TATOA), kuieleza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti nia ya nchi hiyo ikishirikiana na Uganda zilivyokusudia kuachana na mipango yao ya kupitisha mizigo yao katika Bandari ya Dar es Salaam.
Alisema, ni mwendawazimu pekee ambaye anaweza kupitisha mizigo Bandari ya Mombasa kwenda Kigali Rwanda kutokana na umbali uliopo, kwani kutoka Dar es Salaam kwenda Rwanda ni karibu zaidi.
Mwendo wa barabara kutoka Kigali kwenda Mombasa kupitia Uganda ni kilometa 1,704 na hutumia saa 25, tofauti na Bandari ya Dar es Salaam ambayo hutumia kilometa 1,460 na hutumia saa 18 tu kufika Kigali.
Alisema anatarajia hata wakijitoa au wasijitoe, Tanzania itaendelea na juhudi zake za kuimarisha miundombinu ya uchukuzi kwa lengo la kukuza uchumi ikiwemo ya reli, bandari na kuondoa vizuizi 56 vilivyopo na kubakiwa na vitatu.
“Hayo maneno ni ya kwenye vyombo vya habari tu,siamini kama Rwanda wanaweza kuamua kutumia Bandari ya Mombasa ambako pana mwendo mrefu sana tofauti na Dar es Salaam ambako ni karibu na wanatumia saa chache. Tunachofanya sasa ni kuhakikisha tunaondoa vikwazo ikiwemo vizuizi vingi ambavyo ni kikwazo kwa kasi ya uchumi tuitakayo sasa, lakini pia natarajia kukutana na waziri mwenye dhamana wa Rwanda.
“Ni mwendawazimu pekee anayeweza kufikiria kuacha kutumia bandari yetu na kuamua kutumia ile ya Mombasa ambayo ina umbali mrefu zaidi,” alisema Dk. Mwakyembe
Kuhusu sekta ya Uchukuzi, waziri huyo alionya watendaji watakaoshindwa kutekeleza mpango wa Serikali wa kupata matokeo makubwa kwa haraka (Big Results Now-BRN), kwamba wajiandae kufukuzwa kazi kwani hakuna mtumishi ambaye ana ajira ya kudumu ambayo haiwezi kuguswa.
Mbali na hilo, ameonya watendaji wa Mamlaka ya Bandari (TPA), watakaoshindwa kutekeleza Mpango wa Serikali ujulikanao kama Tekeleza sasa kwa matokeo makubwa (BRN), na kusema hakuna mwenye ajira ya kudumu ambayo atashindikana kufukuzwa.
Alisema watendaji wa sekta ya uchukuzi ambao watashindwa kufanyakazi kwa kufuata uhiari wa BRN, basi ajiondoe mwenyewe na akatafute biashara ya chips kwani ndiyo inayomfaa.
Alisema lengo na mpango wa Serikali kwa sasa ni kufufua reli ili kuondokana na usafirishaji wa mizigo mizito kwa njia ya barabara, ambazo ni hatari kwa barabara pamoja na hali ya sasa ya kusafirisha tani 200,000 tu kwa mwaka, ili ifikie tani milioni tatu.
Naye, Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Rais ya Kufuatilia Matokeo ya Mpango wa BRN, Omary Issa alisema tayari wamekwishaanza ufuatiliaji ambapo kila Jumatatu ya kila wiki wizara zilizopo kwenye mpango huo, zinalazimika kutoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu yao kwao.