ACHUNGULIA KABURI BAADA YA KUSHAMBULIWA NA PAPA...

PICHA YA KUSHOTO/JUU: Glen akionesha jereha lake na sehemu ya ubao iliyomegwa na papa huku mwanae akiwa amebeba mfano wa papa aliyemshambulia baba yake. PICHA YA CHINI: Aina ya papa aliyemshambulia Glen.

Anaelezea tukio ambalo hawezi kulisahau pale papa mwenye hasira kali alipozamisha meno yake kwenye mguu wake wa kulia na kunyofoa pande la mnofu.
Glen Folkard alikuwa akielea kwenye ubao wake maalumu wa michezo ya baharini ndipo mnyama huyo mwenye urefu wa mita 10 alipomnasa kutoka kwenye ubao huo aliokanyagia.
Papa huyo, mnyama anayesifika kwa kasi yake ya kunasa binadamu na kudhuru baharini, baada ya kumtupia kwenye maji kabla ya kujiandaa kumrudia na kumng’ata kwa mara ya pili.
Akisimulia jinsi alivyookoa maisha yake, Glen mwenye miaka 44, alipoachiwa akatumia mwanya huo kudandia tena ubao wake huo na kuogelea kwa kasi kuelekea ufukwe wa Redhead, Kaskazini mwa mji wa Sydney huku papa huyo akifuatilia damu iliyokuwa ikichuruzika baharini kutoka kwenye jeraha lake mguuni.
“Aliibuka kutokea chini, akaninasa, akanitupia kwenye maji kisha akanizamisha chini mara kadhaa. Baadaye akaniachia kidogo na hapo ndipo nilipopata mwanya wa kuokoa maisha yangu kwa kudandia kwenye ubao wangu na kuondoka kwa kasi eneo hilo, amesimulia Glen wiki tano baada ya mkasa huo.
Baada ya kufika pwani, Glen ambaye ni baba wa mtoto mmoja, anasema alijitupa mchangani huku mwili wote ukiwa na maumivu na damu ikiendelea kuchuruzika kwa wingi kwenye jeraha.
Aliongeza: Ninachoweza kukumbuka ni kuwa nilijilaza chali kwenye ubao wangu uliokuwa ukielea huku nikitazama angani na kujipongeza, ‘Niko hai, nimefanikiwa’ maana nilikuwa nimechungulia kaburi. Wakati huo yule papa nilishamuacha mita kadhaa baharini akiwa amekata tamaa ya kunipata.
Katika shambulio hilo, Glen amepoteza mnofu unaokadiriwa kuwa na uzito wa kilo nne kutoka mguuni mwake ambapo anaeleza alipoteza damu nyingi kiasi cha kutishia uhai wake.
Baada ya kuokolewa, Glen alilazimika kulazwa siku kadhaa hospitali akiwa chumba cha wagonjwa mahututi kufuatia kupoteza damu nyingi kwenye jeraha lake.
Shuhuda mmoja aliyejitambulisha kama Peter, amesema shambulio hilo la papa lilikuwa kama unaangalia kipande cha sinema.
Alisema wakati wa tukio: “Mwanangu aliniambia kuwa kamuona papa akirandaranda kwenye maji na kumnasa samaki na kuanza kumkokota muda mfupi kabla ya shambulio dhidi ya Glen kutokea.”
“Ngozi ya Glen ilikuwa ya kijivu kabisa. Bila shaka alipoteza kiasi kikubwa sana cha damu.
“Ni kama kuigiza sinema, unajua, tukio mwanzoni lilianza kwa kila mmoja kutoka kwenye maji na kulikuwa na joto sana siku hiyo huku maji yakitamanisha mno kuoga.”
Watu wengi walikuwa wakiogelea huku mamia wakiwa wamejilaza ufukweni ndipo iliposikika kelele kutoka baharini, “Msaada, msaada, niko hatarini,” ikiwa ni sauti ya Glen.
Mcheza michezo ya kwenye maji Steve Tidey anasimulia tukio: “Kulikuwa na pilikapilika kwenye maji, nikageuka na kumwona akirejea ufukweni kutoka baharini.”
“Ubao wake ulikuwa umemeguka huku damu ikichuruzika nyuma yake. Hapo nikatambua kashambuliwa na papa.”
Papa wa aina ile ni wawindaji makini sana na wana kawaida ya kuja mpaka kwenye maji ya kina kifupi. Wanalinda vizuri maeneo yao na kushambulia mnyama yeyote anayevamia mipaka yao.
Wataalamu wanaelezea kuwa Papa 'Chui' na Papa Weupe ndio wanyama wenye kawaida ya kushambulia binadamu.
Imeelezwa kwamba nchini India, Papa wa aina hiyo hufika hadi Mto Ganges na kushambulia binadamu.
Anasema, Glen alianza kupoteza dira mara baada ya kupigwa na wimbi kisha kusombwa hadi eneo la shambulio.
Mara baada ya taarifa zake kusambaa, madaktari wasio na mipaka walifika eneo la ufukweni na kumpatia Glen huduma ikiwamo hewa ya oksijeni katika harakati za kuokoa maisha yake kabla ya kumpeleka hospitali ya jirani kwa matibabu zaidi.
Tidey anasimulia ujasiri wa Glen kwamba licha ya maumivu aliyokuwa nayo, alimudu kutania pale alipoulizia ubao wake wa kuogelea akisema ndicho kitu chake cha muhimu zaidi maishani mwake, mara tu baada ya madaktari kumpatia oksijeni.
Hili lilikuwa shambulio la kwanza la papa kwenye ufukwe uliozungushiwa nyavu maalumu mjini New South Wales tangu Februari 2009 pale muogeleaji mmoja alipokatwa mkono wake na papa eneo la Bondi.
Haijafahamika hata hivyo kama nyavu kwenye ufukwe wa Redhead uliondolewa na mamlaka za bandari au la.
Mpango wa nyavu za kudhibiti papa katika The New South Wales unajumuisha zaidi ya fukwe 50 zenye ukubwa wa eneo unaofikia zaidi ya maili 200 za kipande cha kati ya kaskazini na kusini mwa mjini wa Sydney.
Kuna mfululizo wa nyavu fupi zilizotandazwa kutoka ng’ambo moja ya ufukwe mpaka nyingine kwenda kina cha takribani futi 50 kwenye maji.
Chama cha Green kinachoongoza eneo hilo, kimetoa wito kuondolewa nyavu hizo kwa kuwa zimekuwa hazina tija na zaidi zimekuwa kikwazo kwa ukuaji wa sekta ya uvuvi na viumbe wa baharini.
Gazeti la Sidney Morning Herald lilimnukuu Mbunge wa Chama cha Green, Cate Faermann akisema kuwa nyavu hizo za kuzuia papa si chochote bali ni kero kwa waogeleaji.
“Nyavu zinatakiwa kuwa kizuizi cha papa kufika kwenye maji ya kina kifupi, lakini badala yake zaidi ya nusu ya papa wanavuka na kufika Pwani,” alisema mbunge huyo.
“Nyavu hizo zimekuwa zimekuwa tatizo kwa kusababisha vifo vya maelfu ya kasa, dolphin na viumbe wengine wa baharini ambao hawana hatari yoyote kwa maisha ya binadamu.
Lakini Kitengo kinachoshughulikia Dolphin cha New South Wales kimekanusha madai hayo.
“Tangu kuanza kutumika kwa nyavu hizo mwaka 1937 kuna tukio moja tu baya lilosababishwa na uwepo wa nyavu hizo ufukweni,” ameainisha msemaji wa kitengo hicho’
Msemaji huyo ameongeza: “Kama dolphin watatu na kasa watatu tu wamekuwa waninasa kwenye nyavu hizo kwa mwaka, wakati zaidi ya asilimia 60 ya viumbe wengine wanakwama na kunasuliwa wakiwa hai.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item