JE, WAJUA? MESSI NDIYE MWANASOKA ANAYELIPWA ZAIDI
https://roztoday.blogspot.com/2012/03/je-wajua-messi-ndiye-mwanasoka.html
Mshambuliaji wa Barcelona, Lionel Messi ameongeza utamu kwenye tuzo na medali zake alizopata kwa kutangazwa mwanasoka anayelipwa zaidi duniani kwenye orodha iliyotolewa hivi karibuni.
Mwanasoka huyo aliyeshinda mara tatu Tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka duniani, ameibuka kidedea kwenye orodha hiyo kwa kuweza kujikusanyia mapato yanayofikia Pauni milioni 27.4 kutokana na mishahara, bonasi na matangazo ya biashara.
Nyota huyo wa Barcelona amekusanya kwa mwaka Pauni milioni 13 kutokana na mishahara klabuni hapo pamoja na mikataba ya matangazo ya kampuni za Adidas na Pepsi.
Messi amempiku nahodha wa zamani wa England, David Beckham kwenye nafasi ya kwanza kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na Jarida la FOOTBALL la Ufaransa.
Beckham mwenye miaka 36, amejikusanyia Pauni milioni 26 na kuendeleza umaarufu wake licha ya kuhamishia shughuli zake Marekani kwenye klabu ya LA Galaxy.
Nafasi ya tatu imekwenda kwa mshambuliaji wa Real Madrid, Cristiano Ronaldo ambaye amejikusanyia Pauni milioni 24, licha ya kuongoza kwa kupachika mabao kwenye La Liga akiwa amefunga mabao 32 katika mechi 26 alizocheza msimu huu.
Mshambuliaji wa Manchester United, Wayne Rooney alikuwa mchezaji anayelipwa zaidi kwenye Ligi Kuu England akijikusanyia Pauni milioni 17. Rooney amejikusanyia Pauni milioni 8 kwa msimu katika miaka yake mitano ya mwanzo katika mkataba wake. Licha ya kukumbwa na misukosuko na Coca-Cola mwaka jana kufuatia matatizo ya nje ya uwanja, bado mvuto wake kibiashara kwa makampuni ya England haujatetereka.
Kocha wa Real Madrid, Jose Mourinho alikuwa kocha anayelipwa zaidi akiweka kibindoni Pauni milioni 12.3. Carlo Ancelotti wa Paris St Germain yeye ameshika nafasi ya pili akiweka kibindoni Pauni milioni 11, huku nafasi ya tatu ikienda kwa Pep Guardiola wa Barcelona aliyeweka kibindoni Pauni milioni 7.88.
ORODHA KAMILI NI KAMA IFUATAVYO: £27.5m Lionel Messi (Barcelona)
£26.2m David Beckham (LA Galaxy)
£24.3m Cristiano Ronaldo (Real Madrid)
£19.4m Samuel Eto'o (Anzhi)
£17.2m Wayne Rooney (Man United)
£15.7m Sergio Aguero (Man City)
£14.7m Yaya Toure (Man City)
£13.9m Fernando Torres (Chelsea)
£12.9m Kaka (Real Madrid)
£11.9m Philipp Lahm (Bayern Munich)
