MAHAKAMA YAAMURU FREEMAN MBOWE AKAMATWE...
https://roztoday.blogspot.com/2012/09/mahakama-yaamuru-freeman-mbowe-akamatwe.html
Freeman Mbowe
Mahakama ya Wilaya Hai mkoani Kilimanjaro, imeamuru Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe (Chadema), akamatwe kwa kushindwa kufika mahakamani hapo kujibu tuhuma zinazomkabili za kufanya vurugu kwenye kituo cha uchaguzi mkuu.Mbowe ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chadema, anakabiliwa na tuhuma za kumjeruhi Msimamizi wa kituo cha uchaguzi wakati wa uchaguzi mkuu mkuu uliofanyika Oktoba 31 mwaka juzi.
Hati hiyo ilitolewa mahakamani hapo, baada ya Mbunge huyo kutohudhuria mahakamani hapo pamoja na mdhamini wake bila taarifa zozote.
Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Denis Mpelembwa aliagiza kutolewa kwa hati hiyo, baada ya Mwendesha Mashitaka wa Polisi, Inspekta Marwa Mwita kutoa maelezo ya kutohudhuria kwa mtuhumiwa mahakamani hapo, jambo ambalo ni ukiukwaji wa masharti ya dhamana.
Mwendesha mashitaka alisema, pamoja na kutoa hati ya kumkamata mshitakiwa huyo, pia alitoa hati ya kumkamata mdhamini wake kutokana na kushindwa kufuata masharti ya kumdhamini mtuhumiwa huyo.
Mbowe katika mashitaka hayo, anadaiwa alimshambulia msimamizi huyo, Nasri Othmani na kumsababishia maumivu makali mwilini.
Katika kesi hiyo, anadaiwa kuvunja Sheria ya Makosa ya Jinai kwa kufanya shambulio hilo katika kijiji hicho saa 11 jioni. Kesi hiyo ilipangwa kusikilizwa tena Septemba 18 mwaka huu, kwa upande wa mashitaka kuendelea kutoa ushaidi wake.
