KESI YA OFISA FEKI WA IKULU YAAHIRISHWA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/01/kesi-ya-ofisa-feki-wa-ikulu-yaahirishwa.html
Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam. |
Hakimu Genivitus Dudu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, aliahirisha kesi hiyo jana kwa kuwa Wakili wa mshitakiwa, Mruge Karoli hakufika mahakamani bila kutoa taarifa.
Awali, Wakili wa Serikali Charles Anindo alidai kuwa kesi imekuja kwa ajili ya kuendelea kusikiliza ushahidi wa upande wa mashitaka na jana walikuwa na mashahidi wawili.
Hakimu Dudu alipohojiwa kuhusu wakili Mruge, Taki alidai yupo Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, hata hivyo hakimu alisema haiwezekani kwa kuwa mahakama hiyo iko likizo.
Taki anakabiliwa na mashitaka 27 ya kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, ambapo mashitaka 13 ni ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na 14 ya kughushi.
Anadaiwa kughushi risiti mbalimbali za Serikali, zikionesha kuwa zinatoka kwa Katibu Mkuu wa Wizara ya fedha. Desemba 2, 2009, alighushi hundi ya Serikali namba 39705072 kuonesha kuwa ilikuwa inatoka kwa Katibu huyo.
Aidha anadaiwa kujipatia zaidi ya Sh milioni 100 na Dola za Marekani 2700 kutoka kwa watu na kampuni mbalimbali kwa madai kuwa yeye ni Ofisa Mwandamizi wa Ikulu na Mwenyekiti wa Mamlaka ya Uchapishaji wa Vitambulisho vya Taifa (NIDA) jambo ambalo si kweli.
Anadaiwa Desemba 17, 2009 akiwa jijini Dar es Salaam alijipatia Sh milioni 8.6 kutoka kwa Albert Shuma na Paul Moshi, ambao ni wakurugenzi wa kampuni ya Allyson's Traders na pia alijipatia fedha kutoka katika makampuni na watu wengine.