WALIMU 28,746 KUAJIRIWA MWEZI HUU...
https://roztoday.blogspot.com/2013/01/walimu-28746-kuajiriwa-mwezi-huu.html
Rais Jakaya Kikwete. |
Mpaka sasa Tanzania ina upungufu wa walimu 57,177 katika shule za Serikali, tatizo ambalo imeahidi kulimaliza katika miaka michache ijayo kutokana na idadi kubwa ya walimu wanaofundishwa katika vyuo mbalimbali nchini.
Rais Jakaya Kikwete alitangaza juzi mjini hapa, kuwa kati ya walimu hao, 14,600 watakuwa wa shule za msingi, 14,060 wa sekondari na wengine 80 wa vyuo vya ualimu.
Akihutubia maelfu ya wananchi wa mjini hapa katika siku ya pili ya ziara yake ya kikazi Tabora, Rais Kikwete alisema mikoa yenye uhaba mkubwa wa walimu itapewa kipaumbele katika mgawo huo.
Tabora ni moja ya mikoa yenye uhaba mkubwa wa walimu, ukiwa na upungufu wa walimu 2, 055 na Igunga pekee ikihitaji walimu 285.
Hii itakuwa mara ya pili mfululizo kwa Serikali kuajiri na kusambaza idadi kubwa ya walimu katika jitihada za kumaliza ukosefu wa walimu nchini ambao unachangia matatizo ya elimu nchini.
Mwaka juzi, Serikali iliajiri na kusambaza walimu 24,621, kati yao 11,379 walikuwa wa shule za msingi, 13,246 wa sekondari na 42 wa vyuo vya elimu.
Wakati shule za Serikali nchini zikiendelea kukabiliwa na upungufu wa walimu, shule binafsi zina ziada ya walimu.
Takwimu zinaonesha kuwa shule binafsi za msingi zina ziada ya walimu 2, 857 na za sekondari ziada ya walimu 459 hali ambayo inayojionesha katika matokeo mazuri ya mitihani kwa wanafunzi wa shule hizo.
Rais Kikwete aliwaambia wananchi kuwa Serikali pia inakabili ipasavyo matatizo mengine katika sekta ya elimu ikiwa ni pamoja na ukosefu wa maabara, nyumba za kutosha za walimu na ukosefu wa vitabu.
Kuhusu huduma ya maji nchini, akisema Serikali imeonesha jitihada za kukabiliana na ukosefu wa maji katika maeneo kadhaa ya Tanzania.
Kwa mfano hapa, Rais Kikwete alisema kuzinduliwa kwa mradi wa maji wa Bulenya juzi katika mji wa Igunga na vijiji vitatu vinavyozunguka mji huo, kutakuwa na upatikanaji wa maji wa asilimia 70.
Aliahidi kuwa asilimia 30 iliyobaki itapatiwa majawabu na mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria ambayo yatavutwa kwa ajili ya matumizi ya wakazi wa miji ya Nzega, Igunga na Tabora na vijiji ambako mabomba ya mradi huo yatapitia.
Rais Kikwete ambaye aliwasili mkoani Tabora juzi, jana mchana aliondoka Igunga kuanza ziara ya Wilaya ya Nzega.