VIJANA ZAIDI YA 160 WATAPELIWA AJIRA ZANZIBAR...

Vuai Ali Vuai.
Vijana zaidi ya 160 wametapeliwa fedha na madalali wanaouza ajira katika ofisi nyeti za Serikali hasa zinazohusu ulinzi na usalama.
Matapeli hao wamekuwa wakiuza ajira za Idara ya Usalama wa Taifa, Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Polisi na vikosi vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ).
Tayari vijana hao wamewasilisha malalamiko yao katika taasisi mbalimbali za Polisi, SMZ na ofisi za CCM Kisiwandui.
Akizungumza na vijana waliotapeliwa ajira Kisiwandui mkoa Mjini Magharibi jana, Naibu Katibu Mkuu wa CCM, Zanzibar, Vuai Ali Vuai alisema ajira za Serikali katika vyombo vya ulinzi na usalama haziuzwi.
Alisema amefanya mawasiliano na viongozi wa SMZ na kuthibitisha kwamba hakuna taasisi inayotoa au kuuza ajira kwa sasa.
“Nataka kuwathibitisha vijana, kwamba SMZ  na CCM havihusiki katika utapeli huu…kwanza ajira za Serikali na taasisi za ulinzi haziuzwi,” alisema.
Vuai alisema vijana walioathirika wanatoka makundi yenye msimamo tofauti wa itikadi za vyama vya siasa.
“Hawa vijana wanatoka makundi tofauti ya itikadi za vyama vya siasa ... nimewasikiliza na malalamiko yao tumeyapeleka mbele katika vyombo vya uchunguzi,” alisema.
Mmoja wa vijana hao, Salma Juma alidai kutoa Sh 700,000 na kuahidiwa ajira katika Idara ya Usalama wa Taifa. 
“Nimetoa Sh 700,000 kwa ahadi ya kupewa ajira Idara ya Usalama wa Taifa lakini ni miezi saba sasa ajira hiyo haijapatikana,” alidai Salma ambaye alimaliza kidato cha sita mwaka juzi.
Alidai kuwa fedha hizo alimkabidhi mtu aliyejitambulisha kwake kuwa Ofisa wa Usalama wa Taifa mwenye dhamana ya ajira hizo na aliahidiwa kuajiriwa Julai mwaka jana.
Juma Salum,  alidai kutoa Sh 300,000 kwa ahadi ya kupewa kazi Polisi. “Mimi nimetapeliwa Sh 300,000  ambayo ni ahadi ya kupewa kazi ya upolisi…fedha hizo zilitolewa na wazazi wangu kwa matumaini ya kupata kazi,” alisema.
Mwanamke ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake, alidai kuwa alitapeliwa Sh 200,000 kwa ahadi ya kupewa kazi katika vikosi vya ulinzi vya SMZ hasa Kikosi Maalumu cha Kuzuia Magendo (KMKM).
“Nimetoa fedha hizo kwa ahadi kwamba nitapewa kazi ya Jeshi na kwa vile nilikuwa nahitaji ajira nililazimika kutoa,” alisema.
Vijana hao walidai kubaini wametapeliwa baada ya madalali hao kuwapigwa chenga.
Uchunguzi wa mwandishi kwa vijana hao ulibaini kuwa ajira inayosakwa zaidi na vijana hao ni kutoka Idara ya Usalama wa Taifa ambayo huuzwa na matapeli hao kwa Sh 700,000.
Ajira inayofuatia kwa kupendwa na vijana hao ni za JWTZ ambayo matapeli hao wamekuwa wakichukua  Sh 500,000 na kufuatiwa na Polisi inayolipiwa Sh 300,000.
Ajira zinazohitajika lakini si kwa wingi kama nyingine ni za Vikosi vya Serikali ya Mapinduzi ambazo huuzwa kati ya Sh 200,000 na Sh 100,000.
SMZ ina vikosi vya ulinzi vitano vya KMKM, JKU, Valantia, Zimamoto na vyuo vya mafunzo ambavyo hutunza wahalifu wa makosa mbali mbali katika Magereza ya Unguja na Pemba.
Baadhi ya vijana hao walisema wametoa taarifa Polisi kuhusu utapeli huo huku wakitaja baadhi ya watu waliohusika.
Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Ali Mussa alithibitisha na kusema tayari Polisi inachunguza tukio hilo.
Mussa alisema Polisi imeunda timu kuchunguza tukio hilo ambapo wamepewa taarifa na vijana walioathirika na utapeli huo.
Hivi karibuni JWTZ lilifanya mchakato wa usaili wa ajira kwa vijana katika ofisi za wakuu wa wilaya Unguja na Pemba.
Kutokana na wimbi kubwa la vijana kumaliza shule na kukosa ajira, imekuwa rahisi kurubuniwa wakati wanapoambiwa ajira zipo na kutakiwa kupeleka fedha za maandalizi ya kazi.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item