ALIYEMUUA PADRI EVARIST MUSHI AKAMATWA ZANZIBAR...

Marehemu Padri Evarist Mushi.
Jeshi la Polisi limesema anayedaiwa kuwa muuaji wa Padri Evarist Mushi amekamatwa na ametambuliwa na watu walioshuhudia tukio hilo.

Kauli hiyo ya Polisi inakuja siku moja baada ya Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo kulilaumu Jeshi la Polisi kwa kuzembea kuwakamata watuhumiwa wa mauaji ya padri huyo.
Akizungumza Dar es Salaam juzi, Kardinali Pengo alisema mauaji hayo yamefedhehesha si tu Wakatoliki bali pia Wakristo wote nchini na kusema pamoja na kuwa vitendo hivyo ni vya kinyama, lakini kamwe kanisa halitalipiza kisasi.
Alisema kufuatia mauaji hayo, kanisa limeandaa misa maalumu ya kumuombea marehemu Mushi inayotarajiwa kufanyika Aprili 20,  mwaka huu Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Zanzibar jana, Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa A. Mussa alisema upelelezi wa  kesi hiyo ya mauaji ya Padri Mushi umefikia mahali pazuri.
“Napenda kuwapa taarifa ya maendeleo ya kesi ya mauaji ya Padri Evarist Mushi. Najua si ninyi tu waandishi wa habari lakini Watanzania wote wanataka kujua maendeleo ya upelelezi wa tukio hili.
“Jeshi la Polisi liliwaahidi litawajulisha kila hatua iliyofikiwa juu ya upelelezi wa shauri hili. Mpaka hapa tunapozungumza upelelezi wa shauri hili umefikia pahala pazuri na jalada la shauri hili limeshapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashtaka kwa hatua za kisheria.
“Mhusika wa mauaji haya tayari amekamatwa na ametambuliwa na watu walioshuhudia tukio hilo,“ alisema Kamishna Mussa.
Alisema Jeshi la Polisi lilichukua hatua kadhaa za kiupelelezi,  ikiwa  ni pamoja na kuchora michoro ya sura ya mtu kwa kutumia watu walioshuhudia tukio hilo na kwamba baada ya kuitoa picha hiyo katika vyombo mbalimbali vya kiulinzi, wananchi, vyombo vya habari na mitandao ya kijamii mhalifu huyo ametambulika.
“Jeshi la Polisi liliahidi kutoa milioni kumi kwa watu watakaosaidia kupatikana kwa mhalifu huyu. Ahadi ile ipo pale pale na mwananchi aliyesaidia kutoa utambuzi, Jeshi la Polisi litamzawadia kiwango hicho cha fedha, lakini kwa usalama wa shahidi huyo na kwa sababu za kiupelelezi tukio la kumkabidhi fedha hizo hatutaliweka bayana katika vyombo vya habari.
“Mwisho kabisa, naomba niwashukuru tena wananchi wote wa Zanzibar kwa kuwa karibu na ofisi yangu na Jeshi la Polisi kwa ujumla katika mapambano ya vitendo vya kihalifu,” alisema Kamishna Mussa.
Katika hatua nyingine, Kamishna huyo wa Polisi Zanzibar amewahakikishia amani na utulivu wananchi wa Zanzibar wakati wa Sikukuu ya Pasaka.
“Napenda kuendelea kuwahakikishia uwepo wa usalama na amani kwa muda wote wa mapumziko na Ibada za Pasaka.
“Jeshi la Polisi linawahakikishia kuendelea kudumisha doria za mjini na vijijini kwa kutumia gari, askari wa miguu, pikipiki na mbwa ili kuhakikisha usalama unadumu visiwani hapa.
“Tutaendelea kutoa ushauri wa kiusalama na kushirikiana kwa karibu zaidi na wananchi wote kuona maisha na mali zao zinakuwa salama. Tunawaomba wenye mahoteli ya kitalii na nyumba za starehe kuwa karibu na Jeshi lao la Polisi pamoja na kufuata ushauri wote wa kiusalama wanaopewa kila wakati.”
Naye Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Dodoma, Amon Kinyunyu amesema kuwa sasa watatangaza vita na wale wote wanaotoa vitisho kwa ujumbe wa simu za mkononi kwa viongozi wa dini.
Alisema hayo jana mjini Dodoma wakati wa Ibada ya Ijumaa Kuu iliyofanyika kitaifa katika usharika huo.
Askofu Kinyunyu alisema kuwa vitisho hivyo vimekuwa vikiwaondolea amani viongozi na kuwatia hofu hata waumini wakati wa Ibada za Pasaka. Aliwataka waumini kuwaombea watu hao ili Baba wa Mbinguni aweze kuwasamehe.
“Sasa lazima tutangaze vita. Lazima tuishi kwa amani katika nchi yetu yenye amani ambayo Mungu ametujalia,” alisema Askofu huyo.
Alisema kuwa kwa sasa hali ya nchi si nzuri kutokana na amani kuchafuliwa, watu wamekuwa wakitishiwa maisha na hata kuuawa bila kuwa na sababu huku viongozi wa dini wakiendelea kupokea vitisho.
“Kila jambo baya ambalo linatokea miongoni mwetu Mungu ana kusudi la kuleta jambo jema kupitia jambo baya,” alisema.
Alisema kuwa kifo cha Bwana Yesu kilikuwa na kusudi la kumkomboa mwanadamu, kwani Yesu aliteswa kwa hiari yake bila kulazimishwa ili apate kumkomboa mwanadamu na kila mtu anatakiwa kutafakari kifo cha Yesu katika maisha yake.
Katika mahubiri yake hayo pia aliwageukia viongozi wa kanisa na kuwataka wabadilike na kuwa watumishi wa Mungu kwani wapo baadhi sasa wanaomsulubisha Yesu kutokana na matendo yao.
 Alisema viongozi wengi wa dini wanasema wanamtumikia Mungu lakini ndani ya utumishi wao kuna matendo maovu na watu kama hao wanashiriki kumkana Yesu hadharani.
“Roho ya dhambi iliyo ndani ya binadamu inafanya mtu amkatae Yesu,” alisema.
Pia aliwataka Wakristo kuacha kushiriki kumsulubisha Yesu  kwa matendo yao kinyume na maagizo yake na maagizo ya Mungu katika suala zima la upendo na ujirani mwema.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item