BABA AUA MTOTO WAKE NA KUMZIKA SEBULENI...

Kamanda Diwani Athumani.
Mtoto Debora Riziki (3), mkazi wa kitongoji cha Iponjola katika Kijiji cha Isange wilayani Rungwe, ameuawa na kufukiwa katika shimo ndani ya nyumba ya baba yake mzazi.

Baba yake Debora, Riziki Mwangoka (27), mkazi wa Iponjola, anadaiwa kuhusika na mauaji ya mwanawe huyo,  yaliyogundulika juzi saa 7.40 mchana nyumbani kwake.
Chanzo cha mauaji hayo kimetajwa kuwa ni mgogoro wa ndoa baina ya Mwangoka na aliyekuwa mkewe, Esther Mwambenja (23), anayeishi kwa sasa katika kitongoji cha Kibumbwe, kijijini Kiwira wilayani hapo.
Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Diwani Athumani, alidai jana kwamba wanandoa hao waliotengana katika kipindi kisichojulikana na baada ya hapo, walianza kuvutana wa nani aishi na Debora.
Kamanda Athuman alidai kutokana na ugomvi huo, Novemba 28 mwaka jana saa 11.00 jioni, Mwangoka alimchukua kwa nguvu Debora kutoka kwa mama yake na kuondoka naye kwenda nyumbani kwake.
Alidai baada ya kufika kwake, pasipo huruma wala uchungu na damu yake, Mwangoka alidaiwa kumwua mwanawe huyo na kuchimba shimo katika sebule ya nyumba hiyo na kumzika.
Alifafanua kuwa pasipo hofu yoyote, Mwangoka aliendelea kuishi ndani ya nyumba hiyo, ikiwa na kaburi la mwanawe ndani, hadi juzi ilipogundulika siri aliyoificha katika kipindi hicho chote.
Kwa mujibu wa Kamanda Athuman, baada ya kugundulika kwa kaburi hilo, mwili wa mtoto Debora ulifukuliwa na kupelekwa hospitalini, ambako daktari aliufanyia uchunguzi na kuukabidhi kwa ndugu kwa ajili ya maziko.
Kwa mujibu wa Kamanda Diwani, mtuhumiwa wa mauaji hayo anashikiliwa Polisi wakati utaratibu ukiendelea, ili afikishwe mahakamani.
Wakati huo huo mkoani Mara, mwanamke mkazi wa Kijiji cha Bukanga, Kata ya Makoko, Nyamafuru Patrick (72), ameuawa na watu wasiofahamika juzi Jumanne, kwa kunyongwa shingo.
Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Absalum Mwakyoma, alisema jana kuwa wauaji hao walimnyonga mwanamke huyo kwa kutumia kitenge chake.
Baada ya kufanya unyama huo, alisema walichukua mwili wa marehemu na kuuzika kwenye shimo fupi shambani kwake, huku wakiacha miguu na kichwa vikionekana wazi kwa nje.
Kamanda Mwakyoma alisema kuwa mauaji hayo yalifanyika saa 7.00 mchana, katika Kijiji cha Bukanga, ndani ya shamba la mwanamke huyo, wakati alipokuwa amekwenda kulima.
Mwili wa marehemu kwa mujibu wa Kamanda Mwakyoma, uligunduliwa na familia yake baada ya kufuatilia, kutokana na kuchelewa kurejea nyumbani isivyo kawaida yake.
Baada ya kumfuatilia Nyamafuru na kufika shambani, Kamanda Mwakyoma alisema, familia hiyo ilikuta ameuawa na kufukiwa kwenye shimo fupi katikati ya matuta mawili.
Kutokana na hali hiyo, Kamanda Mwakyoma alisema familia ilitoa taarifa Polisi, ndipo wakafika eneo la tukio na kuchukua mwili wa marehemu na kwenda kuuhifadhi katika Hospitali ya Mkoa wa Mara kwa uchunguzi zaidi.
Uchunguzi wa awali umeonesha kuwa, Nyamafuru  alinyongwa shingo kwa kutumia kitenge alichokuwa amevaa.
“Tunafikiri muuaji hakuwa mmoja, walichimba shimo fupi na kuuzika mwili wa marehemu huku wakiacha kichwa na miguu vikionekana wazi kwa nje,” alisema.
Kamanda Mwakyoma alitoa mwito kwa wananchi kushirikiana na Polisi kutoa taarifa juu ya wauaji hao, ili wakamatwe na kufikishwa mahakamani kujibu tuhuma ya mauaji.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item