BILIONEA WA ARUSHA KUZIKWA KENYA KAMA ALIVYOAGIZA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/03/bilionea-wa-arusha-kuzikwa-kenya-kama.html
Nyaga Mawalla. |
Mgogoro wa maziko ya Wakili Nyaga Mawalla, umeingia katika sura mpya, baada ya wakili wake, Fatuma Karume, kutoa wosia wake ambao ameelekeza azikwe Kenya.
Akizungumza jana jijini Arusha, wakili mwenzake , Albert Msando, alisema Fatuma, ambaye pia ni mtoto wa Rais mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Amani Karume, ndiye aliyeachiwa wosia huo.
Akifafanua kuhusu wosia huo, Msando alisema Nyaga alielekeza katika wosia huo maeneo mawili ya kuzikwa, kulingana na mazingira ya kifo chake.
Kwanza alielekeza kwamba siku akifia Tanzania, azikwe katika shamba lake kubwa la kisasa, lenye mandhari ya hali ya juu, lililopo Momela wilayani Arumeru mkoani Arusha.
Pili kwa mujibu wa wakili Msando, aliyeongozana na Wakili Joseph Naiamanya, Nyaga alielekeza katika wosia huo wa kisheria, kwamba akifa nje ya nchi, maziko yake yafanyike katika nchi hiyo hiyo.
Msando ambaye ni Wakili, aliendelea kusema kuwa kwa sasa ndugu jamaa na marafiki, wako katika vikao vya kawaida na sio vya mvutano, ili kuangalia na kujadili mahali pa maziko na hakuna mvutano kama unavyotafsiriwa na baadhi ya vyombo vya habari.
Kwa mujibu wa Msando, kwa sasa mwili wa marehemu Nyaga, bado uko katika Hospitali ya Nairobi na uchunguzi wa polisi wa nchini Kenya, bado haujakamilika ndio maana mwili huo umechelewa kutolewa majibu ya kiini cha kifo chake.
Kwa mujibu wa wanasheria, ikiwa Nyaga atarejeshwa nchini na ikatokea mtu yeyote kwenda mahakamani kuhoji, Mahakama italazimisha mwili huo urejeshwe Kenya kwa maziko.
Mwanasheria mwingine alisema kwamba wosia wa marehemu ulisajiliwa kwa wakili ni matamshi ya mwisho yaliyojikamilisha ambayo hayawezi kukiukwa kisheria.
Wanasheria waliozungumza na gazeti hili, wamebainisha kuwa akirejeshwa nchini na Mahakama ikiamuru arudishwe Kenya kuzikwa, kutailazimu familia kufuata utaratibu wa itifaki ya Kenya na hivyo kuamsha mgogoro mwingine wa kidiplomasia.
Kutokana na mgogoro huo, taarifa zilizolifikia gazeti hili zimesema kuwa viongozi wa dini na mila, wametumwa kwa wazazi wake, ili walegeze kamba na kukubali maziko ya mtoto wao yazingatie wosia wake.
Vyanzo vya habari kutoka karibu na familia hiyo, vinasema kuwa mdogo wa marehemu, Wilfred Mawalla ametuma viongozi wa dini wakiwemo wachungaji, mapadri na wazee wa mila ya kichaga, kwenda kwa wazazi wake.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, viongozi hao wametakiwa kwenda Marangu kuwaomba wazazi wakubaliane na wosia wa mtoto wao aliouacha akiwa hai.
Tayari mama yake mzazi ambaye jina lake halijapatikana, alishasisitiza kwamba, angependa mwanawe kipenzi azikwe nyumbani kwao Marangu Moshi, na sio mahali pengine popote.
Pia baba yake, Juma Mawalla, ambaye ni Wakili wa siku nyingi, alikaririwa na vyombo vya habari akieleza kuwa hatohudhuria mazishi ya mwanawe, iwapo atazikwa eneo tofauti na Marangu.
Mtoa habari wetu alieleza kwamba kutokana mvutano huo, Wilfred ndipo alipoamua kuwatumia viongozi na dini na mila kwenda kijijini Marangu, kwa lengo la kumlainisha mzazi huyo abadili msimamo wa kutaka maziko yafanyike Marangu.
“Hapa ni kizungumkuti, wazazi wanasema wao ndio wenye kauli ya mwisho ya kuamua na sio wosia ulioachwa, na Wilfred anasema lazima tuheshimu wosia uliachwa na marehemu na ndio maana wametumwa viongozi wa dini na mila kwenda kuwalainisha wazazi wote,” alisema mtoa habari.