BANDARI KUBWA AFRIKA KUJENGWA BAGAMOYO...
https://roztoday.blogspot.com/2013/03/bandari-kubwa-afrika-kujengwa-bagamoyo.html
Wavuvi wakiendelea na shughuli zao kwenye moja ya fukwe za Bagamoyo. |
Mara baada ya kuwasili juzi na kupokea heshima zote za Mkuu wa Nchi, Rais Xi Jinping na mwenyeji wake, Rais Jakaya Kikwete walikwenda Ikulu, ambako walishuhudia serikali mbili hizo zikisaini mikataba 17 yenye manufaa ya moja kwa moja kwa Watanzania na Serikali.
Mkataba mmoja ni wa utoaji wa mkopo usio na riba na mwingine ni wa ujenzi wa Bandari ya Bagamoyo.
Bandari hiyo inatarajiwa kuwa kubwa kuliko zote katika Ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara, na ujenzi wake utatumia dola za Marekani bilioni 10.
China pia imekubali kusaidia Shirika la Utangazaji (TBC), kwa kutoa gari la kurushia matangazo ya moja kwa moja, litakalosaidia kuboresha matangazo yake.
Pia, Serikali na China ilisaini mkataba wa kuipatia Tanzania ushirikiano wa kiufundi na kiuchumi, pamoja na mkopo wenye riba nafuu katika ujenzi wa awamu ya tatu ya Mkongo wa Taifa.
China pia ilisaini hati ya kukabidhi jengo la kisasa la kimataifa la mikutano la Mwalimu Nyerere, ambalo Rais Jinping alilitumia jana kuhutubia dunia kuhusu Sera ya China na Afrika.
Makubaliano mengine yaliyosainiwa kati ya Serikali hizo mbili ni ya kuimarisha ushirikiano katika nyanja za uwekezaji, ikiwemo kutangaza vivutio vya uwekezaji na kulinda uwekezaji wa nchi hizo mbili.
Katika utamaduni, China na Tanzania zilitia saini makubaliano ya utekelezaji wa Programu ya Utamaduni, kati ya nchi hizo mbili kuanzia mwaka 2013 mpaka 2016.
Mbali na utekelezaji wa programu hiyo, pia nchi hizo mbili zilisaini hati ya makubaliano (MoU) ya kuanzishwa kwa Kituo cha Utamaduni cha China nchini.
Katika kilimo, nchi hizo mbili zilitia saini makubaliano ya uhakiki wa ubora wa bidhaa za tumbaku kutoka Tanzania.
Makubaliano hayo yalisainiwa kati ya Shirika la Uhakiki wa Ubora wa Bidhaa za China (AQSIQ) na Wizara ya Kilimo na Chakula. Makubaliano hayo yanatarajiwa kuongeza soko la tumbaku ya Tanzania nchini China.
Mikataba mingine iliyosainiwa kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na China, ni pamoja na Makubaliano ya Ushirikiano wa Kiuchumi na Kiufundi.
Makubaliano mengine ni Hati ya Kuboresha Hospitali ya Abdullah Mzee za Zanzibar na makubaliano ya Kuipatia Zanzibar vifaa vya kukagua makontena bandarini.
Makubaliano mengine ni ya awamu ya kwanza ya ushirikiano wa uendelezaji wa miundombinu ya Wizara ya Fedha, kati ya wizara hiyo na Benki ya Maendeleo ya China.
Pia kuna makubaliano ya utoaji wa fedha, kwa ajili ya miradi mingine ya maendeleo nchini, na makubaliano ya mradi wa kisasa wa viwanda katika ukanda wa kilimo.