MBUNGE AFARIKI DUNIA BAADA YA KUPIGWA NA KIHARUSI...

KUSHOTO: Marehemu Salim Hemed Khamis. KULIA: Baadhi ya wabunge na waandishi wa habari wakisaidia kumbeba Mbunge Salim mara baada ya kuanguka ghafla.
Mbunge wa Chambani, Salim Hemed Khamis (CUF), amefariki dunia.
Mbunge huyo ambaye aliugua ghafla juzi, akiwa kwenye kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, amefikwa na umauti jana saa sita mchana; akiwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, ambako alikuwa amelazwa.

Kwa mujibu wa ratiba ya Bunge, Salim anatarajiwa kuagwa leo saa mbili mpaka saa nne katika Viwanja vya Karimjee Dar es Salaam. Baada ya kuagwa jijini Dar es Salaam, safari itaanza leo saa nne asubuhi kwenda Pemba kwa Maziko.
Salim ni Mbunge wa nne kupoteza maisha tangu kuanza kwa Bunge la Tisa. Mbunge mwingine aliyepoteza maisha ni Godwin Sumari wa Arumeru Mashariki,  Mbunge wa Viti Maalumu Regia Mtema na Mbunge kutoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mussa Salim Silima.  
Kuugua kwa mbunge huyo, kulianza kwa kuanguka ghafla juzi, hali iliyolazimu kubebwa na wabunge pamoja na waandishi wa habari, na kukimbizwa katika hospitali hiyo kubwa nchini.
Kaimu Katibu wa Bunge, John Joel akitoa taarifa ya kifo chake, alisema alipofikishwa hospitalini, alipelekwa kwenye chumba  cha wagonjwa mahututi na baada ya madaktari kumpima alionekana alipatwa na tatizo la kiharusi.
Joel alisema tatizo hilo la kiharusi lilitokana na kupatwa kwa shinikizo la damu, ambalo lilisababisha mishipa ya kichwani kupasuka na damu kuingia kwenye ubongo.
"Alivyofika hospitali hiyo jana (juzi), madaktari waligundua tatizo hilo na walitueleza kuwa wanajitahidi kuiondoa damu hiyo licha ya kuwa ni suala gumu," alisema Joel.
Kabla ya Joel kutangaza kifo hicho, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge wa Mambo ya Nje, Edward Lowassa ambaye alikuwa anaongoza kikao cha Kamati yake, alilazimika kusitisha shughuli za kamati hiyo na kutangaza tukio hilo.
"Ndugu wabunge nina habari mbaya kwenu, nasikitika kutangaza kuwa mwenzetu Salim ambaye aliugua ghafla jana (juzi) hatunaye tena," alisema Lowassa na kueleza kuwa kikao hicho kitalazimika kusitishwa.
''Kifo cha mbunge huyo kimetokea haraka mno kwani hata wakati anapelekwa hospitalini, hakuonesha kuwa na hali mbaya hadi kusababisha mauti yake. Lakini ni kazi ya Mungu haina makosa," alisema Lowassa.
Kwa upande wake, Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta alimwelezea mbunge huyo kuwa alikuwa mtu anayejituma tangu Bunge la Tisa na hasa alikuwa amejikita katika masuala ya kilimo.
"Alikuwa anaulizwa maswali yenye mashiko hasa katika sekta ya kilimo, kwa taifa limempoteza mtu muhimu na CUF wamempoteza mwanachama mahiri," alisema Sitta.
Juzi  mara baada ya mbunge huyo kukumbwa na hali hiyo, alilegea na kukosa nguvu kiasi cha kushindwa kutembea ndipo wajumbe wa kamati hiyo wakiongozwa na Mwenyekiti wake, Lowassa na Makamu Mwenyekiti, Mussa Azzan Zungu walipomtoa nje ya ukumbi na kuanza kumpepea kwa kutumia magazeti na majarida.
Pamoja na juhudi hizo, hali ya mbunge huyo ilizidi kuwa mbaya huku akitokwa na jasho jingi, alizungumza kwa taabu kuwa alikunywa dawa za kuzuia shinikizo la damu, kabla hajala kitu chochote na hivyo kumshinda nguvu.
Kutokana na hali yake kuzidi kuwa mbaya kadri muda unavyokwenda, wajumbe wa kamati hiyo na wabunge wengine wakishirikiana na waandishi wa habari waliokuwemo katika eneo hilo, walimbeba na kumkimbiza kwenye gari kwa ajili ya kupelekwa hospitali.
Mwandishi alishuhudia mbunge huyo akiwa amebebwa na wabunge na waandishi hao zaidi ya 10 kwa kutumia kiti na baadaye walimbeba mwenyewe, lakini wakati wote huo baadhi ya wabunge akiwemo Mbunge wa Kondoa Kusini, Juma Nkamia, walikuwa wakizuia waandishi wasimpige picha.
Waandishi watano walisaidiana na wabunge hao akiwemo Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emmanuel Nchimbi, kumbeba kwa kupitia mlango wa nyuma na kisha kupakizwa kwenye gari la Ofisi ya Bunge lenye namba za usajili STK 2178 aina ya Land Cruiser, ikiongozwa na kusindikizwa na pikipiki ya Polisi PT 2591.
Gari lililombeba Mbunge huyo liliondoka kwenye ofisi hizo saa 5:15 na habari zilizopatikana zilieleza alipelekwa kwenye Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Mchango wa mwisho wa mbunge huyo katika uhai wake, akiwa mbunge  aliichambua  taarifa ya Mpango wa Afrika Kujitathmini Utawala Bora (APRM).
Alitoa mchango wake huo, mwanzoni mwa wiki hii wakati Kamati yake ya Mambo ya Nje, ilipokutana na Menejimenti ya APRM na kujadili taarifa hiyo na hesabu zao za mwaka unaoishia wa 2012/2013.
Alisema kwa upande wake hajafurahishwa na taarifa hiyo ya APRM, kwa kuwa haijagusa maeneo mengi muhimu yanayowagusa wananchi moja kwa moja hasa yale yaliyotawaliwa na tatizo la rushwa.
“Sijui labda mimi ni mgeni katika suala hili lakini katika taarifa hii ya APRM, sijaifurahia kwa kuwa naona haijagusa maeneo muhimu hasa yale ya huduma za moja kwa moja za wananchi kama vile vyombo vya huduma na vyombo vya Dola,” alibainisha.
Alisema katika eneo la vyombo vya Dola kama vile Mahakama na Polisi na katika eneo la vyombo vya huduma kama vile hospitali kwa sasa wananchi wanapata matatizo kutokana na ukweli kuwa vyombo hivyo vimetawaliwa na rushwa.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item