HULKA ZA PAPA FRANCISCO ZAMWEKA MAJARIBUNI KIUSALAMA...

Papa Francis I.
Usalama wa Kiongozi Mkuu wa Kanisa Katoliki Duniani, Papa Francis, unaelezwa kugubikwa na utata kutokana na mtindo wa maisha alionao wa kutaka kuwa huru na karibu na watu, wakati anakabiliwa na tishio la maadui.

Akizungumza na mwandishi hivi karibuni kuhusu usalama wa Papa, Askofu Msaidizi wa Kanisa Katoliki Jimbo la Bukoba, Method Kilaini, alikiri kuwa ipo kazi kubwa katika ulinzi wa kiongozi huyo.
“Papa ni binadamu na ana maadui pia. Ni lazima alindwe si kwamba kwa kuwa ni kiongozi wa kiroho, hivyo hana maadui, hapana, maadui anao,” alisema Askofu Kilaini.
Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu la Dar es Salaam, Eusebius Nzigirwa, naye alizungumzia suala hilo na kueleza kuwa bila shaka kulingana na namna Papa huyo alivyo, walinzi wa Vatican watakuwa wameshajipanga namna ya ulinzi wake.
Ingawa ni muda mfupi tangu achaguliwe kuwa Papa, tayari tabia yake imeelezwa na vyombo vya kimataifa, kuwa inatia shaka katika usalama wake na kuwaweka walinzi wake katika hadhari.
Kwa mfano, siku moja baada ya kuchaguliwa kwake, aliwatoroka walinzi wake waliokuwa katika gari la upapa la kifahari aina ya Limousine, lisiloruhusu risasi kupenya, na kuchukua gari la kawaida kwenda nalo katika hoteli ya kawaida alimofikia, katika barabara zenye harakati nyingi za kibiashara.
Mtaalamu wa usalama wa viongozi wa Uingereza, Richard Aitch, alisema kutoroka walinzi ni hatari.
“Kama kuna mtu anataka kuthibitisha kuwa Papa hana ulinzi wa kutosha, mazingira ya kutoroka walinzi ni hatari,” alisema Aitch. 
Katika Misa ya Jumapili ya kwanza tangu achaguliwe, kabla ya Siku ya Misa ya Uzinduzi wa Kiti cha Upapa Jumanne,  Papa Francis alikwenda kuzungumza na watu waliokuwa wamesimama kwenye geti la Vatican, kushikana nao mikono na kuingia katikati yao.
Siku ya Misa ya Uzinduzi wa Kiti cha Upapa, Papa Francis alisimama kwa karibu nusu saa katika gari la wazi, akibusu watoto na kuwabeba na kuna wakati, alishuka kwenye gari hilo na kwenda kumbusu na kumbariki mlemavu aliyekuwa katikati ya watu wengi.
Tayari amepewa jina la ‘Papa asiyetabirika’, ambalo kiusalama, jina hilo limetafsiriwa kuwa ni hatari.
Gazeti la Italia; La Stampa, lilimkariri mmoja wa wasaidizi wake akilalamika “kama mambo hayatarejea  katika hali ya kawaida, tuna matatizo.”
Msemaji wa Vatican, Federico Lombardi, amenukuliwa wiki iliyopita akisema wanafahamu tabia ya  Papa Francis, ya kupenda kuwa huru karibu na watu na kwamba hatua sahihi za kiulinzi zitachukuliwa.
Ametajwa pia kuwa na tabia ya kuchelewa katika matukio, ambapo Jumapili iliyopita, mmoja wa walinzi wake alionekana kumwomba afanye haraka kutoka kwenye Misa, wakati yeye akiendelea kuzungumza na watu.
“Kila Papa huja na matakwa yake na hakuna wa kumlazimisha kufanya jambo, si ajabu mkasikia Papa karejea kupanda mabasi kama alivyokuwa akifanya Argentina.
“Huyu ni mtu tofauti sana, kazi kubwa ni kwa walinzi, kwa sababu ya hali ya dunia sasa,” alifafanua Askofu Kilaini.
Ingawa Papa kiimani hulindwa na Mungu dhidi ya maadui, lakini pia ni kiongozi wa Serikali ya Vatican. Maadui wa mapapa walianza kujitokeza wakati wa Papa wa kwanza,  Mtakatifu Petro.
Petro aliuawa na Kaisari Nero mwaka 67 Baada ya Kristo, ambaye alichoma moto Roma na kumsingizia  Petro na wenzake.
Baada ya kusingiziwa, Petro alihukumiwa kwa kesi ya uhaini. Alichagua kusulubiwa kichwa chini miguu juu, ili ajitofautishe na kifo cha Yesu Kristo.
Kuanzia wakati huo, viongozi wote wa Kanisa na wafuasi waliokuwa wakitetea imani ya kikristo, waliuawa hadi kabla ya mwaka 313 AD.
Kuibuka kwa mtawala wa Roma aliyeitwa Costantino, kati ya mwaka 313 na 314, kulikuwa mwisho wa mauaji ya kasi dhidi ya watetezi wa imani ya kikristo. Huyu alikubali kuwa Mkristo na kusitisha mauaji.
Hata hivyo, hatari ya kuuawa Papa iliibuka tena Februari 11, 1798, wakati Papa Pius VI, alipotekwa na Jenerali Berthier wa Jeshi la Napolioni la Ufaransa, akiwa katika shughuli zake za upapa Italia. Alikufa akiwa njiani kupelekwa Ufaransa baada ya kutekwa.
Papa mwingine kunusurika kifo ni Papa Paulo VI, Novemba 27, 1970. Alishambuliwa kwa kisu katika uwanja wa ndege wa Manila, Ufilipino, alipokwenda kwa ziara za kikazi. Hakudhurika sana katika shambulio hilo.
Kama hiyo haitoshi, Papa Yohana Paulo II alinusurika kifo baada ya kupigwa risasi Mei 23, 1981 na raia wa Uturuki, Malmet Ali Agca, wakati akihutubia katika viwanja vya Kanisa Kuu la Mtakatifu Petro. Papa alitangaza kumsamehe mtu huyo.
Lakini pia Papa Yohana Paulo II, mwaka 1982 alinyatiwa na mtu aliyetaka kumwua kwa kisu Fatima, Ureno.
Papa mstaafu, Benedict XVI, naye alipata tatizo la kiusalama mwaka 2008 baada ya kijana kuvamia gari alilopanda aina ya Jeep, ingawa alidhibitiwa na polisi wa Vatican. 
Miaka miwili baadaye, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa akili, aliwapita wanausalama wa Papa katika Misa ya Krismasi na kumvuta Papa na kumwangusha chini, ingawa hakujeruhiwa. 

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item