WAFUASI WA SHEKHE PONDA WAHUKUMIWA KIFUNGO CHA MIAKA MITATU JELA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/03/wafuasi-wa-shekhe-ponda-wahukumiwa.html
Wafuasi wa Shekhe Ponda wakisikiliza hukumu yao Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam jana. |
Wafuasi 53 wa Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu, Shekhe Issa Ponda, wamehukumiwa kifungo cha miaka mitatu jela na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya maandamano bila kibali.
Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, alitoa hukumu hiyo jana, baada ya kuridhika na ushahidi uliotolewa na mashahidi 10 wa upande wa mashitaka.
Washitakiwa hao wanadaiwa kufanya maandamano kwa lengo la kumshinikiza Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP), atoe dhamana kwa Shekhe Ponda na Shekhe Swalehe Mukadam, wanaokabiliwa na kesi ya jinai katika mahakama hiyo.
Hakimu Fimbo alisema washitakiwa walikutwa na hatia ya makosa matatu, na katika kila kosa watahukumiwa kifungo cha mwaka mmoja jela na hivyo watatumikia adhabu hiyo kwa wakati mmoja, sawa na kifungo cha mwaka mmoja.
Akisoma hukumu hiyo jana, Hakimu Fimbo alisema upande wa mashitaka ulithibitisha mashitaka
matatu dhidi ya washitakiwa, isipokuwa mashitaka ya uchochezi ambayo walishindwa kueleza ni jinsi gani washitakiwa walishawishi wenzao.
Aidha, alisema mahakama haikubali ushahidi wa washitakiwa, kwa sababu hawakuthibitisha
utetezi wao kuwa walikamatwa wakienda kununua bidhaa, isipokuwa Waziri Toy, ambaye alipatikana na hatia ya kosa moja la kushiriki vurugu.
Hakimu Fimbo alisema aliyekuwa Kaimu Kamanda wa
Polisi, Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Ahmed Msangi, alithibitisha kupokea barua kutoka kwa Shura ya Maimamu na Jumuiya na Taasisi za Kiislamu ya kuomba kufanya maandamano ya amani na kuwakataza kupitia barua na vyombo vya habari.
Alisema licha ya kukatazwa kufanya maandamano, washitakiwa walikusanyika baada ya Swala ya Ijumaa, na baadhi yao walikamatwa na vielelezo, yakiwamo mabango na vipeperushi vya kuhamasisha maandamano hayo.
Awali upande wa utetezi uliiomba mahakama kuwapunguzia adhabu washitakiwa au kuwahukumu
kifungo cha nje, kwa kuwa ni kosa lao la kwanza na wamekaa mahabusu tangu Februari 15 sawa na mwezi mmoja.
“Naomba mahakama iwasamehe au itoe adhabu ndogo kwa sababu washitakiwa wengine wana familia zinazowategemea.
“Pia katika sherehe ya Siku ya Sheria, Rais na Jaji Mkuu walisema wafungwa magerezani ni wengi, hivyo tuipunguzie Serikali gharama za kuhudumia watu wengi,” alidai Wakili wa Utetezi, Mohamed Tibanyendera.
Akizungumza nje ya mahakama, Wakili Tibanyendera alidai kuwa hawajaridhika na hukumu hiyo na wana kusudio la kukata rufaa.
Baada ya hukumu hiyo baadhi ya watu waliokuwa mahakamani hapo, waliangua vilio huku mama
aliyekuwa amebeba mtoto akilia: “Mume wangu umeniacha masikini nitafanya nini miye”.
Ilidaiwa kuwa Februari 15 katika Wilaya ya Ilala Dar es Salaam, washitakiwa walikula njama ya kutenda kosa na kukusanyika bila uhalali, jambo lililosababisha uvunjifu wa amani.
Katika mashitaka mengine, wafuasi hao wanadaiwa kuwa siku hiyo walishiriki vurugu na kukaidi amri halali ya Polisi iliyowazuia kuandamana.
Wakati wafuasi hao wakihukumiwa, Shekhe Ponda alipanda kizimbani kujitetea na kupangua mashitaka yote yanayomkabili.
Shekhe Ponda na wenzake 49 wanakabiliwa na mashitaka ya uchochezi, kuingia kwa nguvu na kujimilikisha isivyo halali kiwanja cha Chang’ombe Markazi kinachomilikiwa na kampuni ya Agritanza na wizi wa mali zenye thamani ya Sh milioni 59.
Akijitetea mbele ya Hakimu Mkazi Victoria Nongwa, Shekhe Ponda alidai kuwa hakuna shahidi wa upande wa mashitaka, aliyeieleza mahakama kuwa alipanga njama na kuwashawishi Waislamu kufanya kosa.
Alidai kuwa hawakuingia kwa nguvu na kujimilikisha eneo la Chang’ombe Markazi, bali walikubaliana na wakurugenzi wa Agritanza kujenga Msikiti wa muda, kama ishara ya kuonesha kuwa eneo hilo halitatumika vingine.
Alidai kuwa Oktoba mosi mwaka jana katika Msikiti wa Mtambani Magomeni, alifanya mkutano na wakurugenzi wa kampuni hiyo kuwaeleza kuwa walipata kiwanja hicho isivyo halali na kukubaliana kuwa atawatafutia kiwanja cha ekari 40 Mkuranga, ili waondoke Markazi.
Alidai alifanya hivyo kwa sababu kulikuwa na mgogoro baina ya Waislamu wakitaka eneo hilo
lirudishwe kwa sababu limeshauzwa zaidi ya mara nne.
Aidha, alidai kuwa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) halikuwa na haki ya kuuza eneo hilo, kwa sababu si mmiliki na lilibadilishana kiwanja hicho na eneo la ekari 40 la Kisarawe mkoani Pwani kwa njia isiyo halali.
Alifafanua kuwa kiwanja hicho ni mali ya Waislamu, kilichopatikana mwaka 1964 kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu na kilimilikiwa na Jumuiya na Taasisi za Waislamu wa Afrika Mashariki, hadi mwaka 1968 jumuiya hiyo ilipofutwa na mali zake kuchukuliwa na Serikali.
Shekhe Ponda alidai kuwa katika shughuli za ujenzi yeye alihusika kutoa taarifa kwa maimamu wa misikiti ya Temeke, kuhamasisha Waislamu kujitolea kujenga Msikiti eneo hilo kuanzia Oktoba 12 hadi 14 mwaka jana walipokamilisha.
Katika mashitaka ya wizi wa vifaa vya ujenzi, Shekhe Ponda alidai kutoiba na kwamba hata Mkurugenzi wa Agritanza alipotoa ushahidi mahakamani alidai kuwa, hakuna mali iliyoibwa, bali zilitumika kwenye ujenzi.