SASA MUME AWEZA KUMNASA KIBAO MKE MBELE YA KADHI...

Waislamu walipoandamana kushinikiza uwepo wa Mahalama ya Kadhi.
Upungufu uliopo katika Mahakama ya Kadhi Zanzibar, umesababisha Serikali kuamua kuifanyia marekebisho sheria iliyoanzisha Mahakama hiyo.


Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, amesema mchakato wa kuifanyia marekebisho Sheria ya Mahakama ya Kadhi, upo katika hatua nzuri.
Alisema hayo jana, alipozungumza katika mkutano uliowakutanisha wanachama na viongozi wa Chama cha Wanasheria Wanawake (ZAFELA), na wataalamu kutoka nchi za Kiislamu, zenye muundo wa Mahakama ya Kadhi duniani, ikiwemo Singapore, Malaysia na Indonesia.
Akifafanua zaidi, Makungu alisema Mahakama ya Kadhi zilizopo zimebainika kuwa na upungufu ambao ni kikwazo katika kuleta ufanisi wakati wa kuhudumia wananchi.
Aliyataja baadhi ya mambo ambayo yapo katika hatua za marekebisho, kwamba ni pamoja na sifa za uteuzi wa Kadhi.
Alisema katika muundo wa sasa, Mahakama ya Kadhi hazina nguvu na meno ya kumuita mtu mahakamani na ikiwezekana kumpa adhabu kama ilivyo Mahakama za Wilaya na Mkoa.
Alitoa mfano kwamba, kwa sasa mume anaweza kumnasa kibao mke mahakamani, mbele ya Kadhi na asichukuliwe hatua yoyote.
"Hizo ndiyo baadhi ya kasoro, ambazo tumeziona zinahitaji kufanyiwa kazi katika Mahakama ya Kadhi, ili kuleta ufanisi na kuwa tegemeo kwa wananchi mbalimbali wenye matatizo yao," alisema.
Mwanasheria na Mtendaji wa ZAFELA, Hamisa Omar alisema Mahakama ya Kadhi inahitaji marekebisho makubwa, ili itoe haki kwa makundi mbali mbali, ikiwemo wanawake wanaowasilisha malalamiko yao hapo.
"Chama cha Wanasheria Wanawake, kimekuwa kikipokea malalamiko mbalimbali kutoka kwa wanawake, pamoja na watoto, kutokana na Mahakama ya Kadhi kushindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu," alisema.
Alitoa mfano katika mirathi, kwamba Mahakama hizo zimekuwa zikiwabana wanawake katika kuwapatia mali, hasa pale wanapofiwa na waume zao, wakati wao ndio wanaoachiwa mzigo wa malezi ya watoto.
Akigusia mabadiliko yanayotarajiwa kufanyika, ili kuleta ufanisi katika uendeshaji wa Mahakama hizo, Makungu alisema ni pamoja na kubadili vigezo na sifa za uteuzi wa kadhi.
"Jaji wa Mahakama Kadhi, atalazimika kuwa na Shahada ya Kwanza ya Chuo Kikuu...tunataka kuhakikisha majaji wenye sifa, ndiyo watakaoongoza Mahakama ya Kadhi kwa ajili ya kuleta ufanisi," alisema.
Pia alisema Mahakama za Kadhi zitapewa nguvu za kisheria, ambapo zitakuwa na uwezo wa kumuita mtu yeyote kwa mujibu wa kosa alilotenda, na ikiwezekana kupewa adhabu.
Zanzibar ni miongoni mwa nchi za mwanzo katika Bara la Afrika na Arabuni, kuanzisha Mahakama ya Kadhi kwa ajili ya kutoa huduma kwa Waislamu.
Miongoni mwa kazi na majukumu ya Mahakama ya Kadhi, ni kusimamia masuala ya mirathi kwa Waislamu, pamoja na kutatua migogoro ya ndoa na talaka na kutoa suluhu.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item