TRAFIKI AGONGWA NA KUFA KWENYE MSAFARA WA KIKWETE...

Wasamaria wakifunika mwili wa Koplo Elikiza mara baada ya ajali hiyo jana.
Askari wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Koplo Elikiza, jana ndiyo ilikuwa siku yake ya mwisho duniani kwani alikufa huku akiwa kazini akihakikisha usalama wa msafara wa Rais Jakaya Kikwete, Dar es Salaam.

Koplo Elikiza alikuwa eneo la Bamaga wilayani Kinondoni akiongoza magari ya msafara wa Rais aliyekuwa katika ziara ya kikazi jijini humo wakati huo ukitoka eneo la Sayansi kuelekea Mwenge na aligongwa na gari lililounganisha msafara huo.
Tukio hilo lililosababisha mauti yake, lilitokea baada ya msafara wa Rais kupita na ndipo gari lililomgonga lilipojiunga kwa kasi ile ile ya magari ya msafara (yaendayo kasi ya takriban kilometa 130 kwa saa) na alipobaini si la msafara, aliingia barabarani kulisimamisha, lakini kwa kasi lililokuwanayo halikusimama, ambapo lilimzoa na kumrusha pembeni mwa barabara.
Mashuhuda wa ajali hiyo, walisema wakati askari huyo akijiandaa kuvuta magari yaliyokuwa yakitoka Shekilango, dereva wa gari hilo bila kuangalia, aliunganisha nyuma ya msafara wa Rais.
Baada ya tukio hilo, gari hilo aina ya Land Rover Discovery namba T328 DML lenye rangi nyeusi, halikusimama bali liliendelea na mbio kuelekea maeneo ya Mwenge ambako pia askari walishaarifiana juu ya tukio hilo na askari aliyekuwa hapo alijaribu kulisimamisha lakini halikusimama.
Badala yake kwa mujibu wa mashuhuda, lilishika barabara ya Sam Nujoma kuelekea Mlimani City, ambako pia maaskari wa Usalama Barabarani walishataarifiana juu ya tukio hilo, wakasimama barabarani kulisimamisha lakini ikashindikana na badala yake likaendelea na safari kuelekea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam.
Gari hilo ambalo ilielezwa na mashuhuda kuwa lilikuwa likiendeshwa na mtu aliyevalia kiraia huku akiwa na abiria aliyevalia sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), lilitoweka.
Habari zilisema baada ya Koplo Elikiza kugongwa, alichukuliwa eneo la tukio na kukimbizwa hospitalini Muhimbili, lakini gari lililomchukua lilipofika katika Daraja la Selander kwenye Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, alikata roho.
Akizungumzia tukio hilo,  Kamanda wa Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Mohammed Mpinga, alisema lilitokea saa 7.00 mchana, eneo za mataa ya kuongozea magari na chanzo chake kikiwa ni mwendo mkali na  kutoheshimu taratibu za barabara kulikofanywa na dereva aliyemgonga.
Mpinga alisema baada ya askari huyo kujiridhisha kuwa msafara wa Rais umepita, alisimama katikati ya barabara  ili kuruhusu  magari yaliyokuwa yakitoka Shekilango kuingia barabara ya Ali Hassan Mwinyi lakini ghafla aligongwa na gari hilo, lililokuwa linakuja kwa kasi nyuma ya msafara wa Rais. 
Alisema askari huyo alitokwa na damu sehemu mbalimbali za mwili. “Pamoja na kuona kuwa amegonga askari, dereva huyo hakusimama na badala yake alilikimbiza gari kwa mwendo ule ule hadi Mwenge na kuelekea Ubungo akitumia barabara ya Sam Nujoma,” alisema Mpinga.
Kamanda Mpinga aliahidi kuwa Polisi itahakikisha inamtambua mmiliki wa gari hilo na kukamata dereva aliyesababisha mauti ya askari huyo na kumfikisha katika vyombo vya sheria.
“Tunaahidi kumkamata mhusika, tutawasiliana na Mamlaka ya Mapato (TRA) Kitengo cha Usajili wa Magari ili kumpata mhusika, tutatoa taarifa kadri tunavyoendelea,” alisisitiza Mpinga. Mwili wa marehemu Elikiza umehifadhiwa katika Hospitali ya Muhimbili ukisubiri taratibu za mazishi.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item