WANAWAKE SINGIDA WADAIWA NGONO WAWEZE KUCHOTA MAJI...

Foleni ya maji.
Wanawake katika Kijiji cha Sasilo Kata ya Sasilo Wilaya ya Manyoni mkoani Singida wamedai kudhalilishwa kijinsia na hata kufanyishwa ngono ili wapate upendeleo
wa kuchota maji katika visima vilivyochimbwa na jamii ya wafugaji.
Aidha, wengine wamedai wamekuwa wakitandikwa bakora na kuvunjiwa ndoo wakati wakichota maji kwenye visima hivyo.
Wanawake hao walifichua hayo juzi baada ya Kampuni ya Bia nchini (TBL) kukabidhi  hundi ya Sh milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa visima 20 katika kata hiyo.
Katika hali isiyo ya kawaida, wananchi hao walitaka kupiga picha na mfano wa hundi iliyotolewa na kampuni hiyo ili wapate ukumbusho huku wakiitaka TBL kupunguza bei ya bia.
Asnat Masasu aliishukuru TBL kwa kusikia kilio cha wanyonge kwani walikuwa wakitandikwa viboko na wakati mwingine ndoo zao kuvunjwa na wafugaji wa kabila la Kisukuma ambao wameingia katika wilaya hiyo.
Kwa upande wake, Romana Stanslaus alisema kijiji hicho kilikuwa na tabu kubwa ya upatikanaji wa maji hali iliyolazimu kutoka nyumbani alfajiri na kurudi saa sita mchana kutokana na taabu ya maji.
“Ukienda kwenye visima vya Wasukuma mpaka wanyweshe kwanza ng’ombe zao ndipo mruhusiwe kuchota maji,” alisema.
Hata hivyo, Jackson Jeremiah alisema kuwa, licha ya wafugaji hao kuchimba visima karibu na mto ulio katika kijiji hicho lakini wamekuwa na kauli si nzuri.
Akijibu madai hayo ya wanawake wa Kijiji cha Sasili, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Fortunata Nkya alisema kuwa hajawahi kusikia udhalilishaji unaotokea kutokana na ukosefu wa maji katika kijiji hicho.
Alisema kama wanawake hao wamekuwa hawatoi taarifa dhidi ya kupigwa na kufanyiwa vitendo vya ngono, hakuna kiongozi atakayefahamu ukubwa wa tatizo hilo, lakini wananchi walitakiwa kuungana na kuchimba visima kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na si kusubiri watu wengine wachimbe hali iliyosababisha matatizo hayo.
“Nadhani baada ya TBL kutoa fedha kwa ajili ya uchimbaji wa visima tatizo litakwisha na wanawake watakuwa na amani zaidi na watafanya shughuli zao za maendeleo kwa wakati,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Uhusiano na Sheria wa TBL, Steven Kilindo alisema mchango wa kampuni hiyo katika kusaidia tatizo la maji katika kata hiyo ni Sh milioni 60 ambapo visima 20 vitachimbwa katika vijiji vitano vya kata hiyo ambavyo ni Sasilo, Mwitikila, Malampaka na Chisingisa.
Aliwataka wananchi kutunza vyanzo vya maji na hata kutunza visima hivyo ili vitumike kwa muda mrefu na kuondoa tatizo la upatikanaji wa maji katika Kata hiyo.
Kwa mujibu wa mkandarasi anayetekeleza mradi huo Kampuni ya Ilawa Improvement Association, ujenzi huo wa visima utakamilika baada ya miezi mitatu ambapo unatarajiwa kuanza Aprili mosi mwaka huu na mkandarasi huyo ameshalipwa nusu ya fedha za kutekeleza mradi huo.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item