BEI YA CHAKULA SASA KUPUNGUA, KAMPUNI 300 ZAJITOKEZA KUWEKEZA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/bei-ya-chakula-sasa-kupungua-kampuni.html
Vyakula mbalimbali katika meza sokoni. |
Tatizo la ongezeko la gharama za maisha, linalotokana na ongezeko la bei ya chakula nchini, linatarajiwa kupungua baada ya kampuni takribani 300 za uwekezaji wa ndani na nje, kuonesha nia ya kuwekeza katika uzalishaji wa chakula nchini.
Kampuni hizo zimejitokeza kuwekeza katika Mpango wa Kuendeleza Kilimo katika Ukanda wa Kusini mwa Tanzania (SAGCOT), utakaotekelezwa katika mabonde ya Kilombero, Rufiji, Malagarasi na Ziwa Nyasa.
Hayo yamo katika hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, iliyosomwa bungeni jana na Waziri Christopher Chiza.
Wakati Chiza akiwasilisha bajeti hiyo na kutangaza kampuni zilizojitokeza kuwekeza katika mpango huo, Rais Jakaya Kikwete amesisitiza kuwa lengo la Sagcot ni kuzalisha chakula cha kutosha nchini na ziada iuzwe nje ya nchi.
Akizungumza mwishoni mwa wiki wakati wa uzinduzi wa Chama cha Wafanyabiashara na Wenye Viwanda wa Tanzania na Uturuki (ABITAT), Rais Kikwete alisema katika utekelezaji wa mpango huo, hekta 350,000 zitatengwa maalumu kwa ajili ya mashamba yatakayozalisha chakula hicho.
Uzalishaji huo wa chakula kwa wingi, unatarajiwa kupunguza bei ya chakula inayoathiriwa na mfumo wa kilimo cha sasa cha jembe la mkono, kinachotegemea mvua ambapo kukitokea mabadiliko ya hali ya hewa, huathirika na bei ya chakula huongezeka.
Pia wakati huo ambao si wa mavuno, Tanzania imekuwa ikipata njaa katika baadhi ya wilaya, inayotokana na wakulima kuuza chakula chote na kujikuta bila ziada, katika muda ambao si wa mavuno na kusababisha Serikali kutoa chakula kwa bei nafuu na wakati mwingine kukigawa bure.
Kwa sasa mfumuko wa bei kwa kipimo cha kasi ya mabadiliko ya bei za bidhaa na huduma zote zinazotumiwa na kaya binafsi, unaonesha kwamba kwa Machi 2013 mfumuko ulipungua hadi asilimia 9.8, kutoka 10.4 Februari 2013.
“Kupungua kwa mfumuko wa bei wa Machi 2013 kunamaanisha kuwa, kasi ya upandaji wa bei za bidhaa na huduma kwa Machi 2013, imepungua ikilinganishwa na kasi ya kupanda kwa bei kwa Februari 2013,” ilieleza taarifa ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu hivi karibuni.
Hata hivyo, bado katika mizania ya matumizi ya kipato cha Watanzania, iliyopo katika Ofisi ya Takwimu ya Taifa, chakula na vinywaji baridi vimekuwa vikitumia sehemu kubwa ya mapato ya Watanzania.
Kwa mujibu wa mizania hiyo, bidhaa hizo huchukua asilimia 47.8 ya kipato cha Watanzania na hivyo chakula kikipanda bei, huchangia mfumuko zaidi wa bei.
Vinywaji vyenye kilevi na bidhaa za tumbaku hutumia asilimia 3.3, mavazi na viatu asilimia 6.7, nishati, maji na makazi asilimia 9.2, samani, vifaa vya nyumbani na ukarabati wa nyumba asilimia 6.7 na gharama za afya asilimia 0.9.
Usafirishaji hutumia asilimia 9.5 ya kipato, mawasiliano asilimia 2.1, utamaduni na burudani asilimia 1.3, elimu asilimia 1.7, hoteli na migahawa asilimia 6.4, bidhaa na huduma nyinginezo asilimia 4.5
Akizungumzia zaidi Sagcot, Chiza alisema katika utekelezaji wa mpango huo, wanatarajia kuongeza uzalishaji wa mahindi, mpunga na sukari, yanayotumika kwa wingi na familia nyingi kwa chakula, ili kujitosheleza.
Mbali na kujitosheleza kwa chakula, alisema soko la karibu linalokusudiwa ni nchi za Ukanda wa Afrika Mashariki (EAC) na nchi wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (Sadc).
Alisema wizara yake inashirikiana na ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Kituo cha Uwekezaji (TIC), kuainisha maeneo ya uwekezaji.
Uanishaji huo kwa mujibu wa Chiza, unalenga kupata mashamba 16 makubwa kwa ajili ya uzalishaji wa sukari na makubwa tisa kwa ajili ya kilimo cha mpunga.
Alisema kwa kuwa na wakulima wakubwa, wadogo watakuwa na nafasi ya kujifunza na kuwa karibu na pembejeo, mitaji na zana, ili kuongeza uzalishaji.
Hata hivyo, alisema katika uwekezaji huo wakulima wakubwa hawatakuwa mbadala wa wadogo.
Waziri Chiza alisema mashamba mengine makubwa yanatarajiwa kuanzishwa eneo la Mpanga-Ngalimila, Kilombero na Lukulilo, Rufiji.
Akizungumzia uwekezaji katika mashamba ya sukari, Waziri Chiza alisema Serikali inafanya majadiliano na mwekezaji wa Eco-Energy, ili kuwekeza na kuzalisha miwa Bagamoyo itakayozalisha tani 150,000 za sukari, meta za ujazo 11,000 za mafuta ya ethanol na megawati 10 za umeme.
Mradi wa Bagamoyo pia utahusisha uwekaji miundombinu ya umwagiliaji ya hekta 3,000 za wakulima wadogo na 1,500 wa vijiji vya Kiwanga na Matipwili.
Pamoja na kushawishi wawekezaji wakubwa, wizara inakusudia kuzalisha mahindi katika halmashauri nane za Mpanda, Sumbawanga, Mbozi, Mbeya, Iringa, Mufindi, Njombe na Songea.
Katika hilo alisema Wizara imekamilisha rasimu ya kusaidia wakulima kwa kufidia thamani ya mazao yao ya biashara bei inapotetereka katika soko la dunia.
Alisema rasimu hiyo, itajadiliwa na wadau mwezi ujao na baadaye kuwasilishwa serikalini kwa uamuzi.
Mazao ambayo yamekuwa yakipata shida katika soko la dunia ni pamoja na pamba, korosho, tumbaku na kahawa.
Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, kwa mwaka huu wa fedha imeomba Sh bilioni 328.13 ambapo kati ya hizo, Sh bilioni 247.09 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na Sh bilioni 81.04 za miradi ya maendeleo.
Wakati huo huo, Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji, imesema Bajeti ya Kilimo ni ndogo na inasababisha sekta ya kilimo kutochangia kikamilifu ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Kamati hiyo pia ilishauri ruzuku ya pembejeo kwa wakulima ya Sh bilioni 66.32 (kama utaratibu wa vocha utatumika kutoa ruzuku) na Sh bilioni 108.5 (kama utaratibu wa mikopo utatumika), iongezwe.
Kamati hiyo pia ilizungumzia haja ya kuajiri wagani 4,949 na kulipa madeni ya wizara yanayofikia Sh bilioni 20.32. Madeni hayo yanahusisha wazabuni mbalimbali waliotoa huduma kwa mwaka 2010/2011 na 2011/2012.
Wakati huo huo, Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imeihadharisha Serikali kuhusu Sagcot, kwa kuhamasisha wawekezaji wakubwa wa nje na ndani.
Msemaji wa Kambi hiyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Rose Kamili (Chadema), alisema pamoja na kuwa Serikali imekuwa ni lazima uangaliwe ili kuepusha nchi na uwezekano wa kuondoa njaa lakini bila ya kuondoa umasikini kwa wakulima.
Alisema hadhari hiyo inatokana na kwamba uwekezaji katika kilimo, unatakiwa ufanywe kwa wakulima wadogo na wa kati, kwani ndio sehemu kubwa ya jamii inayojihusisha na kilimo.
“Kambi Rasmi ya Upinzani inaitaka Serikali kuwekeza zaidi kwenye kada hizo mbili za wakulima. Aidha, tunaitaka Serikali kuchagua aina ya kilimo kitakachoharakisha kuondoa umasikini kwa wananchi wetu.” alisisitiza
Alisema kutoka na mpango huo, ipo haja Serikali ijifunze India na kuwa na uangalifu mkubwa hasa kwa washirika wa wawekezaji hao, ambao ni kampuni za mbolea na mbegu.
“Maandiko na taarifa mbalimbali kuhusu mpango kama Sagcot nchini India, yanaonesha kuwa wakulima wadogo na wa kati wamekuwa majeruhi wakubwa wa kampuni zinazozalisha mbegu, dawa na mbolea,“ alisema Kamili.
Alisema India ililazimika kusitisha uuzaji wa mbegu za pamba aina ya Bt-Cotton, zilizokuwa zinazalishwa na kusambazwa na Kampuni ya Monsanto, kwani zilikuwa ghali kwa asilimia 100, ikilinganishwa na mbegu za asili.