JALADA LA WILFRED RWAKATARE KUPELEKWA KWA DPP...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/jalada-la-wilfred-rwakatare-kupelekwa.html
Wilfred Rwakatare. |
Upelelezi wa kesi inayomkabili Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama wa Chadema, Wilfred Rwakatare na Ludovick Joseph, umekamilika na jalada lake litapelekwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) kwa hatua zaidi.
Kaimu Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, Issaya Mngulu, alisema hayo jana, wakati akizungumza Dar es Salaam, kuhusu hatua zilizofikiwa katika matukio kadhaa yaliyotokea nchini yakiwamo ya Zanzibar.
Matukio hayo ni pamoja na kumwagiwa tindikali kwa kada wa CCM, Musa Tesha, katika uchaguzi mdogo wa Igunga mwaka 2011.
Mengine ni kuvamiwa na kujeruhiwa kwa Mhariri Mtendaji wa New Habari 2006, Absalom Kibanda, kutekwa na kujeruhiwa kwa Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk Steven Ulimboka na tuhuma za kigaidi zinazowakabili Rwakatare na Joseph.
Kuhusu kumwagiwa tindikali kwa kada wa CCM, Mngulu alisema watuhumiwa wawili, tayari wameshafikishwa mahakamani na upelelezi upo katika hatua za mwisho.
Alisema endapo watabainika watuhumiwa wengine, nao watafikishwa mahakamani.
Kuhusu Kibanda, Dk Ulimboka na matukio yaliyotokea Zanzibar na mengine yaliyoripotiwa katika vituo vya Polisi nchini, Mngulu alisema uchunguzi bado unaendelea.
“Uchunguzi na upelelezi wa matukio hayo upo katika hatua za kiupelelezi, ambazo si vema kuziweka wazi ili kuepusha kuharibu upelelezi unaoendelea,” alisema Mngulu.
Alishukuru wananchi kwa ushirikiano na kusaidia kufanikisha upelelezi wa matukio ya uhalifu, na hatimaye kufanikisha kukamatwa kwa wahalifu. Aliwataka kuendelea na ushirikiano huo, ili nchi iendelee kuwa salama.
“Vilevile Jeshi la Polisi tunaomba kuufahamisha umma na waandishi wa habari, kwamba zipo sheria na taratibu za kutoa habari za matukio yanayoripotiwa katika vituo vya Polisi.
“Ieleweke kwamba taarifa zinazoripotiwa vituoni kwa mujibu wa sheria, ni za siri kwa faida ya wahanga wa kesi na kwa ajili ya kufanikisha upelelezi,” alisema.
Alisema kanuni za Polisi zinaruhusu Kamanda kutoa taarifa za kituo, na si kujadili ushahidi wa kesi ili kuepusha kuathiri mwenendo wa kesi mahakamani.
Alipoulizwa kuhusu kuchelewa kwa upelelezi wa baadhi ya matukio, Mngulu alisema upelelezi kwa kawaida hauna muda maalumu, ila unategemea ushirikiano.
Alisisitiza, kwamba uchunguzi wa tukio lolote unapokamilika mapema au kuchelewa, hutokana na ushirikiano unaopatikana.