GODBLESS LEMA AIBWAGA TENA CCM MAHAKAMANI...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/godbless-lema-aibwaga-tena-ccm.html
Godbless Lema. |
Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, kwa mara nyingine amewabwaga mahakamani wanachama wa CCM, waliokata rufaa katika kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2010, yaliyompa mbunge huyo wa Chadema ushindi.
Mahakama ya Rufaa Kanda ya Dar es Salaam, jana ilihalalisha ubunge wa Lema kwa mara nyingine, baada ya kutupilia mbali ombi la marejeo ya hukumu iliyomrejesha Lema bungeni.
Jopo la majaji watatu wa Mahakama hiyo, likiongozwa na Jaji Engelo Kileo, lilitoa uamuzi huo jana kwa kuwa ombi hilo halikuwa na msingi wa kisheria na kuamuru wanachama hao, kulipa gharama za mawakili wawili.
Lema alivuliwa ubunge Aprili 5 mwaka juzi, katika Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, baada ya kushindwa katika kesi ya kupinga ushindi alioupata katika uchaguzi wa 2010, iliyofunguliwa na makada watatu wa CCM.
Hata hivyo, Desemba 21 mwaka jana, Mahakama ya Rufaa ilimrejesha bungeni Lema, baada kushinda rufaa yake aliyofungua mahakamani hapo, akipinga hukumu iliyomvua ubunge, kwa kuwa waliomshitaki hawakuwa na haki kisheria.
Baada ya ushindi huo wa awali wa Lema mahakamani, wanachama hao, Mussa Mkanga, Happy Kivuyo na Agnes Mollel, hawakuridhika na uamuzi huo na kuiomba Mahakama ifanye marejeo ya hukumu hiyo, ama iandae jopo jipya kusikiliza rufaa hiyo.
Katika ombi lao, wanachama hao walikuwa wakidai kuwa uamuzi huo ulikosewa, na sababu zilizotolewa na majaji, za kuhusisha haki yao ya kisheria ya kufungua kesi ya kupinga matokeo ya uchaguzi, inapingana na uamuzi mwingine wa mahakama hiyo.
Wakili wa wanachama hao, Alute Mughwai, alidai kuwa Mahakama ilikosea iliposema hapakuwa na ushahidi katika kumbukumbu za Mahakama, kuonesha kuwa wao walikuwa ni wapiga kura waliojiandikisha na katika majumuisho yao, walithibitisha hilo.
Aliongeza kuwa Katiba na Sheria ya Uchaguzi, zinampa uhuru mpiga kura kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi, hata kama haki yake haijaathiriwa, lakini katika uamuzi wa rufaa walidai kuwa hawakuwa na haki ya kufungua kesi hiyo.
Alidai kuwa katika rufaa hiyo, Lema aliwasilisha hoja 18 lakini hoja moja ndiyo iliyotolewa uamuzi na kuiomba Mahakama kuamuru uamuzi huo upitiwe upya, na isikilize hoja zilizobaki.
Wakili wa Lema, Method Kimomogoro, aliomba Mahakama hiyo kufuta ombi hilo na kuamuru wanachama hao kulipa gharama za mawakili, kwa kuwa hakuna msingi wowote unaoonesha makosa katika uamuzi wa rufaa hiyo, bali mabishano.
Awali Wakili Mughwai, aliomba ombi hilo lisikilizwe mbele ya jopo la majaji watano, lakini ombi hilo lilitupiliwa mbali.
Desemba 21 mwaka jana, Mahakama ya Rufani ilitengua hukumu ya Mahakama Kuu na ikamthibitisha rasmi Lema kuwa ni mbunge halali.
Mahakama ilieleza kuwa hakukuwa na ushahidi kuwa wanachama hao walikuwa wapiga kura waliosajiliwa, na hata kama ingekuwa hivyo, hawakuwa na haki ya kisheria kufungua kesi kupinga matokeo ya uchaguzi, kwa madai kwamba Lema katumia lugha za matusi kwenye kampeni zake.
Lema alidai kuwa, wanachama hao wamlipe gharama zote za kesi kuanzia Mahakama Kuu na kudai kuwa kabla ya uamuzi huo, hakuwa na wasiwasi na aliendelea na kazi zake za ubunge kwa sababu mawakili wake walimfariji kuwa atashinda.
Akizungumza nje ya Mahakama ya Rufaa jana, Wakili wa Lema, Tundu Lissu alisema kwa mara nyingine Mahakama imekubali kuwa maombi ya makada hao wa CCM, hayana msingi na kuonya wanaotumwa kufungua kesi za ajabu waache.