HII NDIO SIRI YA USHINDI YANGA, WACHEZAJI WAAHIDIWA MILIONI 100 WAKITWAA UBINGWA, ...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/hii-ndio-siri-ya-ushindi-yanga.html
Kikosi cha timu ya soka ya Yanga kilichowasambaratisha maafande wa JKT Ruvu jana. |
Timu ya Soka ya Yanga, jana imeiangushia kipigo cha mabao 3-0 JKT Ruvu na sasa kuhitaji pointi moja tu kuweza kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Mabao ya Simon Msuva, Hamis Kiiza na Nizar Khalfan yaliwahakikishia wababe hao wa Mitaa ya Twiga na Jangwani pointi tatu muhimu katika mbio za ubingwa kutoka kwa watani wao wa jadi, Simba, ambao walishanyoosha mikono mapeema.
Lakini nini hasa siri ya mafanikio hayo ya Yanga msimu huu, hususani katika mzunguko huu wa pili ambapo iliweza kushinda mfululizo na kukalia kiti kwa takribani mzunguko wote huo.
Imebainika kwamba ahadi za 'kufa mtu' walizopewa wachezaji wa Yanga ambazo nyingine zimeshaanza kutekelezwa, ndizo zinazowafanya wachezaji hao wakose usingizi na kuwazia kuwashushia vipigo wapinzani wao.
Kwa mujibu wa chanzo cha kuaminika, wachezaji wa Yanga kwanza wameahidiwa Shilingi milioni 5 taslimu kwa kila ushindi watakaoupata, ambapo chanzo hicho kimeweka wazi kwamba kibopa mmoja aliyeko katika safu ya uongozi amekuwa akitimiza ahadi hizo.
"Hivi ninavyokwambia, kila pointi tatu Yanga thamani yake ni Shilingi milioni 5, na tayari wachezaji wamevuta walipocheza na JKT Oljoro. Jamaa hataki mchezo kabisa katika suala hilo," kilisema chanzo hicho cha habari.
Chanzo hicho kilikwenda mbali zaidi pale kilipofichua kwamba Mwenyekiti wa Yanga, Yussuf Manji ameahidi kutoa Shilingi milioni 100 kwa wachezaji endapo watafanikisha kutwaa ubingwa huo. Hiyo inamaanisha kwamba kila mchezaji atajikusanyia kiasi kisichopungua Shilingi milioni 3.
Imeelezwa pia kwamba safari ya Uturuki imechangia kwa kiasi kikubwa kuibua morali ya wachezaji sambamba na ujio wa kocha mpya, Ernst Brandts, huku wengi wakiamini kwamba katika kufurahia ubingwa, Manji anaweza kuwatangazia neema nyingine sambamba na kambi nje ya nchi kujiwinda kwa michuano ya kimataifa.
"Kila mtu katika Yanga anajituma ile mbaya, maana hakuna cha kusingizia hapa, kama pesa ipo," kilitamba chanzo hicho.
Kuhusu madai kwamba Yanga imekuwa ikinunua mechi, hususani hizi za kufunga msimu, chanzo chetu kilisema;
"Asikudanganye mtu bwana. Nakuhakikishia Manji alishasema kwamba hakuna sababu ya kununua mechi maana uongozi wake umetumia fedha nyingi mno kusajili kwa nia ya kufanya vema."
Aliongeza: "Pamoja na hayo, hali imechafuka sana kwa sasa katika soka letu, Takukuru wapo macho mno kuwasaka wenye vijitabia hivyo kwa hiyo ukinaswa tu ujijue umetolewa kafara."
"Watu wanaosema tunanunua mechi wanatapatapa. Angalia ratiba yetu, mechi karibu tatu tumecheza na Wanajeshi. Utamhonga nani pale?" alimalizia.
Miongoni mwa mechi za kumalizia Yanga imecheza na JKT Oljoro, Mgambo Shooting na JKT Ruvu."
Kwa sasa Yanga imejikusanyia pointi 56 baada ya ushindi dhidi ya JKT Ruvu, na hivyo sasa kuhitaji sare tu katika mechi yake ijayo dhidi ya Coastal Union ya Tanga.
Azam inayoshika nafasi ya pili ikishinda mechi zake zote zilizobaki itafikisha pointi 56 ambazo tayari Yanga inazo.