WABUNGE WAGHUSHI VYETI VYA SHULE, NECTA WACHUNGUZA...

Wabunge wakiwa ndani ya ukumbi wa Bunge.
Wakati wananchi wakilaani vurugu zinazofanyika bungeni, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani, ametaka wabunge waache tabia ya kughushi vyeti vya elimu.

Wabunge hao mbali na vurugu pia, waliwanyooshea vidole watumishi wa umma pekee wanaoghushi vyeti vya elimu, ambapo Waziri Kombani mbali na kukiri kuwapo kwa udanganyifu huo serikalini, lakini alisema hata wabunge wanashiriki.
“Tusiangalie watumishi wa umma peke yao kuwa ndio wanaghushi vyeti vya elimu kwani hata hapa bungeni tupo, na sisi tunaoghushi vyeti vya darasa la saba, kidato cha nne, ninawasihi tuandike vyeti vyetu vya kweli.
“Mimi nilishakuwa Ofisa Utumishi pale Chuo Kikuu cha Dar es Salaam,  ukiangalia cheti cha Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) cha miaka ya 1960 na vyeti vya sasa, ni rahisi kujua aliyeghushi,” alisema.
Hata hivyo, alisema Utumishi inafuatilia walioghushi vyeti kwa kushirikiana na Necta na kusisitiza, kuwa utaratibu huo utachukua muda mrefu kufuatilia walioghushi, wanaotumia vyeti vya waliokufa na wote watachukuliwa hatua za kisheria.
Alitaja baadhi ya taasisi ambazo zinahakikiwa kuwa ni Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) na Magereza. Hakutaja kama Bunge nalo litahakikiwa. 
Wakati Kombani akiumbua wabunge kwa baadhi yao kughushi vyeti, wananchi waliohojiwa na gazeti hili, walielezea masikitiko yao kuhusu vurugu na ukosefu wa maadili ya kitanzania, unaooneshwa na wawakilishi hao wa wananchi.
Mkazi wa Dar es Salaam, Gasper Sango, akizungumza na gazeti hili, alipendekeza kipindi cha Bunge katika televisheni, kianze kwa alama ya 18 kama katika CD za sinema; inayoonesha kuwa hairuhusiwi kuangaliwa na mtu mwenye umri wa chini ya miaka 18, au PG kuonesha lazima mzazi awepo wakati wa kuangalia.
"Tumefikia mbunge anapotoa maneno machafu, tunaona aibu Watanzania lakini wao wanazomea tu, basi ni vizuri Bunge hili liwe kama sinema, kwamba waone watu wazima tu, watoto hawaruhusiwi kuona kutokana na matusi yanayotolewa na hao tunaowaita waheshimiwa," alisema Sango.
Dk Alex Nkayamba wa Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA), katika maoni yake alisema wabunge waliochaguliwa wanabeba uzito wa jamii.
Alisema licha ya kuwa ni watu wazima, bado wamepewa jukumu la kusimamia ustawi na maendeleo ya jamii kwa ujumla wake na pia ni mfano.
Alisema iwapo mtu aliyepewa wadhifa na dhamana ya hali ya juu namna ile, anaamua kutoithamini kwa kutenda ama kuongea yasiyofurahisha machoni mwa watu, tena kinyume na maadili ya jamii yetu, basi mtu huyo amepotea na hivyo hana budi kujirekebisha ama awajibishwe.
Mwanamuziki wa dansi, John Kitime, alisema mwenendo wa Bunge kwa sasa unafadhaisha na kuvunja moyo, kwa sababu badala ya wabunge waliochaguliwa na wananchi kujadili hoja za maendeleo, wanatumia nafasi hizo kutafuta umaarufu.
“Hata ukifuatilia mwenendo wa wabunge, wanachokifanya ni tabia zao ambazo hata kabla ya kuingia bungeni ndivyo walivyokuwa wakifanya walipokuwa kwenye jamii.
“Baadhi yao  walikuwa wakorofi na kuhamasisha vurugu na wengine hata kutafutwa na Polisi kutokana na vurugu zao. Hali hii inatufanya sisi wenye blogu za vichekesho tupate vichekesho vya bure,” alisema.
Mkazi mwingine wa Dar es Salaam, Aggrey Peter, alisema yanayotokea bungeni ni matunda ya chaguo la wananchi.
“Hebu tujiulize kama walikuwa wanatoa maneno machafu wakati wa kampeni na tukawachagua kwa kuona kwamba wanafaa, hatuna haja ya kushangaa, ndiyo matunda ya kura zetu,” alisema kwa masikitiko.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC), ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema chama hicho, hakiwezi kuvumilia vurugu zinazoendelea bungeni na kwamba wanamtaka Spika, Anne Makinda na Naibu Spika, Job Ndugai kuwachukulia hatua wabunge wanaofanya vurugu ndani ya Bunge hilo.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara jana Gairo, Morogoro,  Nape   alisema chama chao kimesikitishwa na vurugu zilizotokea Dodoma na kwamba wanaamini vurugu hizo ni mkakati wa Chadema wa kutaka nchi isitawalike, ndiyo maana wapo tayari kukiuka kanuni na taratibu za Bunge.
“CCM hatufurahishwi na hali ya vurugu zilizotokea bungeni, kwani hii ni dhihaka kubwa kwa Watanzania  ambao wanategemea Bunge kushughulikia matatizo yao ambayo ni mengi na yanahitaji ufumbuzi,” alisema Nape.
Alisema tabia ya wabunge wa Chadema kutafuta umaarufu kwa kugomea taratibu na kanuni halali zinazoendesha na kusimamia shughuli za Bunge, haikubaliki na hiyo inaonesha kuwa wabunge hawako tayari kutumikia Watanzania na badala yake wapo kwa manufaa binafsi.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item