VIGOGO ARDHI WASHITAKIWA KWA WIZI WA SHILINGI MILIONI 1OO...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/vigogo-ardhi-washitakiwa-kwa-wizi-wa.html
Waziri wa Ardhi, Nyumba na Makazi, Prof. Anna Kajumulo Tibaijuka. |
Vigogo watatu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, wamepandishwa kizimbani kwa tuhuma za ubadhirifu na wizi wa Sh milioni 100.
Washitakiwa hao ni Kaimu Mkurugenzi wa Sera na Mipango wa Wizara hiyo, Simon Lazaro, Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi, Gerald Mango na Kaimu Mhasibu Mkuu wa Tume hiyo, Charles Kijumbe.
Walifikishwa mbele ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jana na kusomewa mashitaka manne na Wakili wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Leonard Swai mbele ya Hakimu Mkazi, Aloyce Katemana.
Wakili Swai alidai kuwa kati ya Mei 18 mwaka jana, katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Lazaro akiwa mwajiriwa wa Wizara, aliwasilisha nyaraka za marejesho kwa mwajiri wake, zinazoonesha amepokea Sh milioni 100 kutoka Tume ya Taifa ya Matumizi Bora ya Ardhi.
Katika nyaraka hizo, Swai alidai Lazaro alionesha kutumia fedha hizo kupima ardhi katika wilaya za Babati, Kilolo na Bariadi jambo ambalo si kweli.
Katika mashitaka ya matumizi mabaya ya madaraka, inadaiwa kati ya Julai 4 na Agosti 5 mwaka juzi, washitakiwa wote wakiwa waajiriwa wa wizara hiyo, walitumia madaraka yao vibaya kinyume na Kanuni ya Fedha za Umma ya Mwaka 2004.
Wakili Swai alidai katika mashitaka ya ufujaji na ubadhirifu wa fedha za umma kuwa, kati ya Julai 4 na Agosti 5 mwaka juzi, Lazaro alitumia Sh milioni 100 alizopokea kutoka Tume hiyo kwa manufaa yake binafsi.
Kwa mujibu wa madai ya Swai, fedha hizo zilipaswa kutumika kwa ajili ya kupimia ardhi katika maeneo ya Arusha, Muleba mkoani Kagera, Ngorongoro, Songea, mkoani Ruvuma, Kilosa, mkoani Morogoro na Mpanda mkoani Katavi.
Washitakiwa walikana mashitaka na Wakili Swai, alidai upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na kuiomba Mahakama ipange tarehe ya kuwasomea maelezo ya awali.
Waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya dhamana ambapo, Lazaro alisaini hati ya Sh milioni 50 na kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika ambao walisaini hati ya kiasi hicho cha fedha na barua za utambulisho wa ofisi zinazotambulika.
Mango na Kijumbe walisaini hati ya Sh milioni 25 na wadhamini wawili kwa kila mmoja, ambao walisaini hati ya Sh milioni 10. Kesi hiyo itatajwa Aprili 30, kupangiwa tarehe ya kuwasomea maelezo ya awali.