WATAKIWA KUWASILISHA USHAHIDI KUHUSU MATESO YA USALAMA WA TAIFA....
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/watakiwa-kuwasilisha-ushahidi-kuhusu.html
Mathias Chikawe. |
Serikali imekitaka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kama kina ushahidi wa uhakika kuwa baadhi ya maofisa wa Idara ya Usalama wa Taifa wanashiriki kuteka na kutesa watu, wauwasilishe Polisi.
Waziri wa Sheria na Katiba, Mathias Chikawe alitoa rai hiyo juzi baada ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani, Profesa Kulikoyela Kahigi kutoa hoja ya kuondoa mshahara wa Waziri wa Utawala Bora hadi Serikali itakapokubali kufanya uchunguzi juu ya tuhuma za maofisa hao.
Chikawe alisema mtu mwenye malalamiko aende Polisi ili hatua zichukuliwe, badala ya kufanyia kazi tuhuma zinazoandikwa magazetini.
“Tuhuma hizo zilizotolewa ni maoni ya mtu mmoja na mimi waziri niende wapi, si kwa sababu tuhuma zikisemwa tu bungeni tunafanya uchunguzi, malalamiko yana utaratibu wake na yote yanapelekwa Polisi,” alisema Chikawe.
Chikawe alitoa ufafanuzi huo baada ya Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Halima Mdee wote wa Chadema, kueleza kwa nyakati tofauti kuwa wana ushahidi wa namna maofisa wa taasisi hiyo nyeti wanavyoshiriki kutesa watu.
Mnyika katika maelezo yake, alisema taarifa zilizopo zinaonesha kuwa maofisa hao wamekuwa wakishirikiana na baadhi ya watu kuteka raia na kuwatesa wakiwataja Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania, Absalom Kibanda na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka.
Mdee katika maelezo yake, alisema Serikali haipaswi kukwepa kuchunguza tuhuma hizo, kwani ushahidi uliopo hauna shaka, kuwa taasisi hiyo inajihusisha na vitendo vibaya.
Mwanaseria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema, alisema kama kuna mtu ana ushahidi juu ya vitendo hivyo vinavyodaiwa na baadhi ya wabunge ni vema akafungua kesi dhidi ya suala hilo.
“Bahati nzuri Tanzania tuna sheria ambayo inaruhusu watu binafsi kuendesha mashitaka, hivyo wenye ushahidi wakafungue kesi,” alisema Jaji Werema.
Naibu Waziri wa Nishati na Madini, George Simbachawene, alisema taratibu za kisheria zinaeleza wazi kuwa mtu mwenye tuhuma za matendo ya jinai lazima aziwasilishe Polisi.
“Wenzetu hawa wanapiga kelele hapa bungeni, lakini hakuna kesi yoyote iliyofikishwa Polisi, sasa Serikali itaanza kuchunguza suala hilo kuanzia wapi wakati kwenye vyombo vya uchunguzi hawajalifikisha?” Alihoji Simbachawene.
Profesa Kahigi katika hoja yake hiyo alisisitiza kuwa hataunga mkono suala hilo hadi Serikali ikubali kufanya uchunguzi kama ilivyopendekezwa kwenye hotuba yake.
Hadi mwisho wa majadiliano hayo, Anne Makinda alihoji wabunge kama wanaunga mkono hoja hiyo na wabunge wengi wa CCM wakaipinga.
Wakati huo huo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais (Uhusiano), Steven Wasira ametaka watu wenye kanda zinazochochea udini kuziwasilisha Polisi, la sivyo wakikamatwa nazo watahesabika kuwa miongoni mwa waliokusudia kuleta uchochezi wa kidini nchini.
Akijibu baadhi ya hoja zilizotolewa na wabunge, Wasira alisema ni kweli kuna kikundi cha watu kinasambaza kanda za dini zinazochochea watu wa dini moja kudhuru wafuasi wa dini nyingine ambao wanasakwa na Polisi na baadhi yao wamekamatwa.
Alisema baadhi ya watuhumiwa waliosambaza kanda hizo wametorokea nje ya nchi na Tanzania inaendelea kuwasiliana na Shirika la Kimataifa la Polisi (Interpol) ili wakamatwe na kurejeshwa nchini.
Alisema baadhi ya watuhumiwa hao wa udini walikamatwa Mwanza, Tanga, Simiyu na Dar es Salaam na hatua za kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria zimefanyika.
Kuhusu suala la kuchinja, Wasira alisema linakuzwa kama moto na akasisitiza kuwa Tanzania haina sheria inayozuia mtu kuchinja nyumbani kwake. Alitaka wananchi waheshimiane katika maeneo yao na waende na mfumo unaoimarisha umoja wao.
Alisema suala la udini ni jambo zito na ndiyo maana Serikali imefungia vituo viwili vya redio vya Kwa Neema ya Mwanza na Radio Imani ya Morogoro kwa miezi sita, baada ya kubainika kuwa wanarusha matangazo yenye uchochezi wa kidini.
Akijibu hoja za Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema, ambaye alitumia hotuba yake juzi kumshutumu Rais Jakaya Kikwete kuwa ndiye muasisi wa udini, Wasira alisema urais ni taasisi na uamuzi unaotolewa Ikulu unatokana na ushauri wa Waziri Mkuu na Katibu Mkuu Kiongozi.
Alitaka Bunge ambacho ni chombo kikubwa kujadili suala la udini kwa kukemea kwa nguvu bila kujali tofauti zao za vyama, akisema kauli ya Lema ya kumshutumu Rais ni chafu.
Pia alisema licha ya masuala hayo kuzungumzwa na wanasiasa, wananchi bado wanashirikiana vijijini na mitaani na hakujatokea matukio ya kutengana.
Alisema katika hatua za muda mfupi ambao Serikali imechukua ni kukutana na viongozi wa dini zote, tayari wamekutana na viongozi wa kiislamu na sasa watakutana na viongozi wa kikristo. Alisema baada ya hapo watawakutanisha na wote wana mwelekeo wa kupenda amani.
Aliongeza kuwa pia wana mkakati wa viongozi wa mikoa kufanya mikutano na viongozi wa dini walioko katika eneo hilo, lengo likiwa ni kuhakikisha suala hilo linalozungumzwa kinadharia linapatiwa ufumbuzi wa haraka.
Kuhusu shutuma kuwa Usalama wa Taifa wanashiriki kutesa wapinzani, Wasira alisema chombo hicho hakishiriki kutesa, bali kulinda usalama wa nchi na akatoa mifano kadhaa ya namna chombo hicho kilivyo na kazi nzito badala ya kufuata watu binafsi.
Alisema kwa kuwa Usalama wa Taifa unaimarisha usalama katika nchi, mtu ambaye atatoa kauli za kuvunja utulivu na amani iliyopo na kusisitiza maandamano ni lazima afuatwe na maofisa wa idara hiyo, kuona kama watu wa aina hiyo wana nia ya kuvunja utulivu uliopo.
“Wewe kila siku unahubiri maandamano na kutoa kauli kuwa nchi haitatawalika, ni lazima wakufuate, hivyo wanasiasa wajaribu kushindana kwa kutumia sheria zilizopo na hoja na si kuleta vitendo vya kuvunja amani,” alisema Wasira.