WATANO WAFA KATIKA AJALI YA BASI ULANGA...
https://roztoday.blogspot.com/2013/04/watano-wafa-katika-ajali-ya-basi-ulanga.html
Kaimu Kamanda John Laswai. |
Watu watano wamekufa na wengine 13 kujeruhiwa baada ya basi dogo la abiria linalofanya safari kati ya Ifakara, wilayani Kilombero na Malinyi, Ulanga, mkoani Morogoro kuacha njia na kupinduka katika barabara ya Ifakara-Malinyi.
Kati ya waliokufa, wanaume ni wanne na mwanamke mmoja ambao baadhi yao majina yao yametambuliwa na ni wakazi wa Ifakara na Mahenge, wilayani Ulanga.
Kaimu Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, John Laswai, jana alithibitisha kutokea kwa ajali hiyo Aprili 18 saa 8.20 mchana, eneo la kijiji cha Namhanga wakati basi hilo likitoka Ifakara kwenda Malinyi.
Alitaja gari lililohusika na ajali hiyo kuwa ni basi dogo aina ya Eicher, namba T 972 BVU lililokuwa likiendeshwa na Cheyo Mkwawa (40).
Alitaja waliokufa kuwa ni pamoja kondakta wa basi hilo na mfanyabiashara wa Mahenge, Jerome Assenga (43) na Reuben Kaswela (32), mkazi wa Ifakara. Wengine ni Robert Mbigwa (20), wa Ifakara, Chausiku Nungo (22) wa Kiswago, Malinyi na mwanamume ambaye jina lake halifahamiki anayekadiriwa kuwa na umri wa kati ya miaka 30 na 35.
Mganga Mkuu wa Kituo cha Afya Lupiro, kilichopo makutano ya barabara ya kwenda Malinyi na Mahenge, Dk Wadugu Wadugu alisema alipokea majeruhi kadhaa ambapo mmoja wao alifariki dunia huku akipatiwa tiba kituoni hapo.
Dk Wadugu alimtaja majeruhi huyo kuwa ni Mbigwa na baadhi ya majeruhi walisafirishwa kwenda katika hospitali ya Mtakatifu Francis mjini Ifakara kwa matibabu zaidi.
Mganga Mkuu wa Hospitali ya Misheni la Lugala, iliyoko Malinyi, Dk Moses Mweni, alisema alipokea majeruhi wawili hospitalini hapo.