MBUNGE MACHALI WA NCCR-MAGEUZI ASHAMBULIWA NA VIBAKA NJIANI...

Mbunge Moses Machali akiwa hoi kitandani baada ya kushambuliwa na vibaka jana.
Mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi), Moses Machali amesema alivamiwa na watu wanne ambao walimshambulia na kumjeruhi akiwa meta 30 kabla ya kufika nyumbani kwake.

Akizungumza jana akiwa katika Hospitali ya Mkoa mjini hapa alikolazwa kwa ajili ya matibabu, alisema hajafikiria kama kuna mkono wa siasa kutokana na tukio hilo.
“Sijafikiria kama kuna mkono wa siasa, kwani bado sijaona dalili za mkono wa siasa, nimezoeana na vijana sana, lakini tukio la kunishambulia ni kitu kilichonishtua sana,” alisema Machali ambaye ana jeraha puani huku akitembea kwa kuchechemea.
Tayari Jeshi la Polisi linashikilia watu wawili kuhusiana na tukio hilo ambao ni  Jeremiah Mkude (18) mkazi wa Chadulu mjini hapa, aliyekutwa na jeraha usoni linaloaminika alilipata wakati akipambana na mbunge huyo na vijana waliokuwa wakimsaidia. Mwingine ni Charles Chikumbili (22) mkulima mkazi wa Swaswa.
Akizungumza kwa shida akiwa kitandani huku mara kadhaa akifuta machozi, Machali alisema alikumbwa na mkasa huo juzi jioni wakati akitoka bungeni na alivamiwa  eneo la Area D Makole meta 30 kabla ya kufika nyumbani kwake.
“Niliona vijana wanne wakisimama katikati ya barabara, nikapiga honi ili wanipishe lakini hawakufanya hivyo,” alisema.
Alisema kutokana na hali hiyo aliwahoji sababu ya kusimama katikati ya barabara bila kuhofia kugongwa. “Wakasema wewe mdogo wake na mbunge ni mpumbavu tu huku wakitoa maneno mengi ya kejeli.
“Nikawauliza kama wana ugomvi na mimi hawakujibu kitu na mara nikaona wengine wanazunguka na kuja nilikokuwa nimekaa maana nilikuwa nikiendesha gari mwenyewe,” alisema.
Alisema aliamua kuondoa gari lakini walilipiga, akasimama na kushuka kwenye gari nao wakamfuata.
“Nikasikia mmoja akisema uwe mbunge, shemeji yake mbunge, mshenzi utapigwa tu ndipo wakanishambulia kwa ngumi nami nikajitetea,” alisema mbunge huyo.
Alisema walimpiga tena ngumi akadondosha simu, wakaichukua na mmoja wao akaenda kwenye gari akalizima na kuchukua funguo ndipo akaanza kumkimbiza hali iliyofanya wenzake wamvamie na kumshambulia hadi kuishiwa nguvu.
Machali alisema, hata hivyo vijana wawili wa Chuo cha Biashara (CBE) walimsaidia  kupambana na vibaka hao ambapo mmoja wa wanafunzi hao alijeruhiwa kwa kung’atwa kwa meno na mmoja wa vibaka hao na kufikishwa hospitalini ambako alipata matibabu na kuruhusiwa.
“Nasikia maumivu usoni, mguu wa kulia na kwenye mkono,” alisema Mbunge Machali.
Alifanyiwa vipimo vya X-ray jana asubuhi na alikuwa anasubiri majibu. Pia alishukuru Jeshi la Polisi kwa kumsaidia na kutaka ulinzi uimarishwe katika maeneo mbalimbali ya mji huu.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa, David Misime alithibitisha kutokea kwa tukio hilo   juzi eneo la Area D.
“Alikutana na vijana wanne waliosimama katikati ya barabara akapiga honi lakini hawakupisha. Aliwahoji sababu ya kuwa katikati ya barabara wakamjibu kuwa anajifanya mtoto wa mbunge na kwamba watampiga,” alisema Misime.
Alisema askari walipowakamata na kuwapekua watuhumiwa hao usiku wa manane, walikutwa na misokoto miwili ya bangi.

Post a Comment

emo-but-icon

Follow Us

Hot Reads

Recent

Comments

Side Ads

Traffic

Text Widget

Connect Us

item